Na Beatrice Sanga-MAELEZO

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umesema utaendelea kuimarisha huduma zake kwa wateja ili kuongeza ufanisi na kupunguza urasimu na muda wa malipo kwa wanufaika wa mfuko huo.

Hayo yameelezwa leo August 31, 2023 na CPA Hosea Kashimba, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa PSSSF wakati wa Mkutano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, PSSF na wahariri wa Vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam ambapo amebainisha kuwa kwa sasa Mfuko huo umepunguza muda wa malipo kwa pensheni ya kila mwezi, ikiwa ni wastani wa shilingi billioni 67 hulipwa kwa wastaafu kila ifikapo tarehe 25 ya mwezi husika ambalo ni ongezeko la asilimia 100 ukilinganisha na kiasi cha wastani wa shilingi bilioni 34 wakati mfuko huo unaanzishwa.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa kwa sasa Mfuko huo umepunguza muda wa kusubiri Mafao kutokana na kwamba Mfuko unalipa ndani ya siku 60, kwa mujibu wa sheria, ilihali kabla ya kuanzishwa kwa Mfuko huo wastaafu wengine walitumia zaidi ya miaka 3 kusubiri Mafao yao, vilevile Mfuko huo tangu kuanzishwa kwake umefanikiwa kulipa madai mbalimbali yaliyorithiwa kutoka kwenye Mifuko iliyounganishwa.

“Kiasi cha Shilingi 1.03 trilioni kililipwa ndani ya miaka miwili kwa zaidi ya wanufaika 10,273, lakini pia thamani ya Mfuko imeongezeka kwa asilimia 27.76 kutoka TZS 5.83 trilioni hadi TZS 8.07 trilioni, kwa sasa Wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wanalipwa kwa kanuni inayofanana.” Amesema CPA Kashimba.

Aidha Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa mpaka sasa kiasi cha TZS trilioni 8.88 kimelipwa kwa wanufaika na wengi wao wakiwa ni wastaafu katika makundi ya Mafao ya Uzeeni/Kustaafu, TZS Trilioni 4.63 (52.19%), Pensheni ya kila mwezi TZS Trilioni 3.31 (37.26%), Mafao ya Kifo TZS billion 461.72 (4.69%), Mafao ya kuacha kazi TZS billion 350.99 (3.95%), Mafao ya Elimu TZS billioni 5.56 (0.06%), Mafao ya uzazi TZS billion 57.76 (0.65%), Mafao ya Ugonjwa TZS billion 7.97 (0.09%), Mafao ya kukosa ajira, TZS billioni 5.80 (0.07%), Malipo ya Michango TZS billion 92.24 (1.04%)

Vilevile Mfuko huo umeendelea na shughuli za uwekezaji katika miradi ya Ubia ili kujiongeza mapato ambapo imebainishwa kuwa uwekezaji huo utaongeza fursa ya kuongeza ukwasi katika Taasisi za fedha na kuwezesha wananchi kupata mikopo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo na kiuchumi, kuongeza ajira, kodi serikalini na kukuza mitaji

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF Bw. Deodatus Balile akizungumza na kutoa shukurani sake kwa. Uongozi wa PSSSF

CPA Kashimba amesema miongoni mwa Miradi ya ubia na wawekezaji wengine kwenye Sekta ya Viwanda, ni pamoja na Kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro kilichopo Moshi, Mkoani Kilimanjaro, PSSSF (86%) na Jeshi la magereza (14%), Awamu ya Kwanza ya Kiwanda hiki ilizinduliwa Octoba, 2020, Machinjio ya Kisasa ya Nguru Hills: PSSSF (39%), Eclipse Investment LLC (46%), na Busara Investment LLP (15%), Kiwanda cha kuchakata Tangawizi cha Mamba Myamba, PSSSF (65%) na Ginger Growers Rural Cooperative Society (MGGRCS) (35%), na Kiwanda cha Chai cha Mponde PSSSF (42%), WCF (42%), na ofisi ya Msajili wa Hazina (16%).

“Mfuko umefanikiwa kuongeza thamani ya uwekezaji kwa asilimia 23.5, kutoka TZS trilioni 6.40 hadi TZS trilioni 7.92, wastani wa ongezeko la asimilia 4 kila mwaka, lakini pia mfuko umepata mapato yatokanayo na uwekezaji ya wastani wa asilimia 85 kwa mwaka, pamoja na kuwaunganisha Wafanyakazi wote waliotoka kwenye Mifuko minne iliyokuwa na utamaduni tofauti, kuandikisha Wanachama wapya 140,162 kwa wakati ikiwa ni waajiriwa wa Serikali na Taasisi zake, ambapo kwa sasa idadi ya wanachama kwenye Mfuko ni 731,183, wanaume wakiwa ni 434,667 na wanawake ni 296,516.” Amefafanua CPA Kashimba.

Katikati ni James Mlowe Memeja Uhusiano na Elimu kwa Umma Eric Mkuti Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina na kushoto   ni Memeja wa PSSSF Dar es Salaam Ufo Swai.

Mfuko huo umejipanga kuhakikisha huduma zote zinafanyika kwa njia ya mtandao ifikapo 2024 ambapo kwa sasa ni asilimia 90, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inatumiwa na Mfuko huo katika kazi zake lakini pia kuwekeza zaidi katika kuendeleza rasilimali watu ili kuongeza ubunifu na ufanisi katika utendaji, kuimarisha ushirikiano wa kikazi na Taasisi washirika katika utoaji wa huduma, kuendelea kupunguza muda unaotumika kulipa Mafao kutoka siku sitini za sasa hadi kufikia siku zisizozidi 30.

Mfuko wa PSSSF, ulianzishwa mwaka 2018 kupitia sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi, Sura 371, ambapo ni matokeo ya ya kuunganishwa kwa Mifuko ya GEPF LAPF, PPF, PSPF, ili kuleta uendelevu wa Mifuko, kuondoa ushindani uliokuwa hauna tija kwa Mifuko kushindania wanachama wachache waliokuwa wanaingia katika soko la ajira ikilinganishwa na idadi ya Mifuko iliyokuwepo.

By Jamhuri