Putin anakuja Tanzania

LICHA ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kusuasua kuthibitisha kuhusu ujio wa Rais wa Russia, Vladimir Putin taarifa za uhakika zinasema kwamba mwamba huyo wa kimataifa atatua nchini Februari, mwakani.
Chini ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Tanzania imekuwa ikitembelewa na viongozi mbalimbali wa kimataifa hususani wa Ulaya, Marekani na Asia.
Taarifa kutoka vyanzo vya uhakika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, zinasema kwamba kuna mchakato unaendelea juu ya ujio wa Rais huyo anayeongoza taifa lake kibabe.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alikataa kudhibitisha taarifa ya ujio  huo, lakini alieleza kuwa yeye atasafiri kuelekea Moscow mwezi ujao kwa mwaliko wa heshima uliotoka kwa waziri mwenzake wa Mambo ya Nje, Sergei Lavrov.
Membe alisema hakuwa na taarifa yoyote inayohusu ujio wa Putin wala maandalizi ya ziara hiyo, “kama ipo, basi itafahamika baada ya ziara yake.”
Kadhalika Membe alilieleza gazeti la kila siku linalochapishwa kwa Kiingereza, “Ninachoweza kukwambia kwa wakati huu ni kwamba nimealikwa Moscow mwezi ujao. Ni lazima niende, na nitakuwa mtu pekee katika nafasi ya kusema chochote juu ya mjadala wetu.”
Ubalozi wa Urusi uliopo jijini Dar es Salaam ulisema hauwezi kuthibitisha juu ya ziara hiyo kwa kuwa hawakuwa na taarifa yoyote kutoka Moscow.
“Ninachofahamu ni kwamba Waziri wetu wa Mambo ya Nje alikutana na mwenzake wa Tanzania New York wakati wa kikao cha Baraza la Usalama. Ziara unayozungumzia inaweza ikawa moja kati ya mambo waliyoyajadili,” alisema Ofisa Mkuu wa Ubalozi wa Russia nchini.
Ziara ya Putin inakuja baada ya miaka miwili tangu Tanzania imepokea viongozi wakuu wa mataifa yenye nguvu duniani – Rais wa China XI Jinping aliyeitembelea Tanzania mwezi Machi mwaka jana na Rais wa Marekani Barack Obama miezi mitatu baadaye.
Muda na vikwazo vya kisiasa vya ziara ya kiongozi wa Urusi kwa Tanzania ni jambo ambalo tayari limeibua maswali kutoka wataalamu wa masuala ya Uhusiano wa Kimataifa na Waangalizi wengine.
Moja ya jambo ambalo liko wazi ni kwamba kuna uwezekano wa Putin kutumia fursa ya ziara hiyo kuhamasisha uhusiano imara wa kiuchumi na kisiasa wa nchi hizi mbili ambao awali uliwanufaisha kabla ya kuanguka kwa  Ujamaa mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Pia Wataalam wanasema, Tanzania ambayo inapambana kuendeleza sekta yake ya gesi na mafuta baada ya ugunduzi wa hazina kubwa ya gesi asili, ina nafasi nzuri za kunufaika kutoka kwenye ziara ya kiongozi wa nchi yenye utaalamu mkubwa kwenye eneo hilo.
Kwa upande mwingine wanasema kuwa, Putin atataka kupata baadhi ya makubaliano ya kibiashara kwa ajili ya kampuni za gesi na mafuta za Urusi kwa  wakati huu ambao nchi za Afrika Mashariki zinakabiliwa na matatizo ya ndani na vikwazo vya uzaaji nje ya nchi.
Mwisho.
Kikwete awakoroga wagombea urais
Na Mwandishi Wetu
KAULI mbili zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete juu ya kushika wadhifa huo mkubwa nchini, zimewachanganya baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliotangaza na wale wanaotajwa kuwania kumrithi.
Rais Kikwete akiwa ziarani China, ametangaza kwamba “kazi ya urais ni ngumu” na kwamba kwa upande wake anatamani amalize kipindi chake miezi 10 ijayo ili aingie kwenye mashambani yake akalime. Kuna wakati alipata kusema angependa akistaafu afundishe.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete aliitoa jijini Beijing, China mbele ya mabalozi wa Afrika wanaowakilisha mataifa yao nchini China waliokusanyika kwenye Nyumba ya Wageni wa Serikali ya China ya Diaoyutai.
Hii ni kauli ya pili yenye tafsiri ya utata iliyotolewa na Rais Kikwete kwani siku chache kabla ya ziara hiyo aliwaasa vijana kumchagua mtu, “anayefanana na kijana” kurithi nafasi yake katika Uchaguzi Mkuu 2015 kiasi cha kuwaibua wahusika ambao wamezungumza kauli tofauti.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira ameibuka akisema: “Nataka hiyo kazi ngumu. Mimi nasema wacha watu wote wajitokeza, tutapimwa wote tunaotaka urais halafu wanachama wa CCM na wananchi wataamua wa kumpa kazi ngumu. Mimi naiweza.”
Alisema kwamba angependa wajitokeze vijana, wanawake na wazee ili kuchujwa kabla ya kupatikana yeye kwa kuwa ana uzoefu wa kazi ngumu.
Kwa upande wake Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangallah amesema: “Hiyo kazi ngumu lazima apewe kijana. Ndiyo maana Rais Kikwete amesema kwamba ni wakati wa vijana. Tunachangamkia fursa hiyo.”
“Mimi niliishasema kwamba Rais Kikwete yuko sahihi. Sidhani kama mzigo mzito ni wa kumpa mzee. Itakuwa ni kumuumiza,” anasema Dk. Kigwangallah na anaungwa mkono na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye pia ameshatangaza nia kama Dk. Kigwangallah.
“Ni kupokezana. Ni zamu ya vijana,” alisema Makamba huku Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja akisema: “Maneno ya Rais Kikwete ni ya kuyaheshimu sana hasa kwa wakati huu taifa likitaka damu changa. Nchi hii kubwa inataka mtu anayeweza kukimbiakimbia.”
Mbali ya hao wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo nyeti ni pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Pia wamo Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohamed Gharib Bilal.