Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Njombe

Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi, amewataka wananchi kupuuza upotoshaji wa taarifa unaofanywa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya watu na vyombo vya habari visivyofuata maadili ya kazi kuhusu misaada inayotolewa kwa waathirika wa maporomoko ya tope yaliyotokea wilayani Hanang, mkoani Manyara.

Bw. Matinyi ametoa rai hiyo leo mjini Njombe katika mkutano wa mkuu wa mkoa akiwa na Wakurugenzi wa Halmashauri na Waandishi wa Habari unaoratibiwa na Idara ya Habari (Maelezo) kwa lengo la kutangaza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

“Mambo yanayoandikwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu upotevu wa misaada ya Hanang si ya kweli; na kwamba wananchi waliopokewa katika kambi walifikia 689 kutoka kaya 139 na kwa hiari yao wenyewe waliomba warejee kwa ndugu zao au makwao kwa sababu wengine hawakupoteza nyumba bali ziliharibika au ziliingia tope,” alisema Bwana Matinyi.

Aidha, amearifu kwamba Rais Samia Suluhu Hassan alisema baada ya tathmini serikali itawajengea nyumba watu wote waliopoteza nyumba zao katika maafa haya.

“Kila mwananchi aliye kwenye kambi anapewa uhuru wa kuamua na akiondoka anapewa misaada stahiki ambaoo katika awamu ya kwanza kila aliyeondoka alipewa chakula cha kutosha siku 30, vifaa na vitu binafsi na vya ndani lakini tumekwenda awamu ya pili ambapo kila walioacha maelezo yao wanapelekewa misaada kwenye kata wanapoishi na wanapewa vitu vinavyotosha kwa muda wa miezi sita,” amearifu Bw. Matinyi.

Aliongeza kwamba waathirika hao wanapewa vyakula vya kutosha miezi sita na kwa sukari ni inayotosha kwa matumizi ya miezi 19; kuna unga wa uji wenye virutubisho kwa ajili ya watoto, majiko, sabuni, magodoro, na vitu vingine vingi vya ndani isipokuwa samani.

Msemaji Mkuu aliongeza zaidi kuwa hata wale ambao hawakuhamia kambini nao wamesaidiwa chakula na vitu muhimu na kwamba misaada ya chakula na vitu imefikia shilingi bilioni mbili.

Alisema pia fedha zilizokusanywa hadi kufikia tarehe 20 Desemba, 2023, ni shilingi bilioni 5.2 akieleza fedha hizo zimeingizwa kwenye akaunti moja ya maafa inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

By Jamhuri