Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amezielekeza halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kuzalisha miche ili kuongeza nguvu katika zoezi la upandaji.

Amesema hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua vitalu vya miche inazalishwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Jiji la Dodoma pamoja na vikundi katika eneo la Mailimbili leo Desemba 21, 2023.

Dkt. Jafo amezitaka mamlaka hizo za serikali za mitaa zaidi ya 180 kuwatumia wataalamu wa miti TFS ili kuzalisha miche kwa wingi ambayo inahitajika kwa kiasi kikubwa ili kufikia lengo la upandaji miti milioni 1.5 kwa mwaka kwa kila halmashauri.

Pia, amezielekeza halmashauri kutumia maeneo ya pembezoni mwa barabara zishirikiane na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara Mijiji na Vijijini (TARURA) kuandaa vitalu ili kupendezesha miji.

Aidha, Waziri Jafo amewataka wananchi kutumia mvua za vuli zinazonyesha katika baadhi ya maeneo nchini kuelekea masika kwa kupanda miti kwa wingi kama ambavyo viongozi wakuu wameelekeza.

“Nimefarijika kutembelea maeneo haya yanayozalisha miche hii ya miti mbalimbali na nawapongeza sana TFS pamoja na vikundi vya kijamii vinavyojishughulisha na uzalishaji wa miche kwani si tu wanasaidia upatikanaji wa miche lakini pia wamejitengenezea ajira,” amesema.

Halikadhalika Dkt. Jafo amesema kuwa maelekezo ya Serikali ni kupanda miti hivyo zimeanzishwa kampeni mbalimbali ambazo zinahamasisha upandaji wa miti

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Kanda ya Kati TFS Mathew Kiondo amewahimzi wananchi kujitokeza kwa wingi kuchukua miche ili waipande na kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.

Amesema pamoja na Wakala huo kuzalisha miche na kuigawa bila malipo kasi ya miwitikio wa uchukuaji wa miche bado ni ndogo kwani kati ya milioni moja ni 200 tu imeshagawiwa kwa wananchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akikagua vitalu vya miche inayozalishwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Jiji la Dodoma pamoja na vikundi katika eneo la Mailimbili leo Desemba 21, 2023.

“Tuna malengo ya kuibadilisha Dodoma kuwa nya kijani na ndio maana ili kuongeza kasi ya uzalisha wa miche tumeanzisisha greenhouse (kitalu nyumba) hivyo tunawaomba mje kwa wingi mchukue miche mkaipande,” amesisitiza Kiondo.

Naye Afisa Mazingira wa Mkoa wa Dodoma Salvatory Mashamba ametoa wito wa uonglozi wa jiji hilo kutenga maeneo ya wazi na kuwagawia wadau ili watayariushe vitalu.

Pia, amewashukuru TFS kwa utaraibu wao wa kuzalisha miche kisha kuigawa bure kwa wananchi hatua inayosaidia kuhakikisha upatikanaji wa miche unakuwa wa uhakika hivyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza wakati wa ziara ya kukagua vitalu vya miche inayozalishwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Jiji la Dodoma pamoja na vikundi katika eneo la Mailimbili leo Desemba 21, 2023.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akifurahia jambo na wanakikundi cha uzalishaji a miche alipofanya ziara ya kukagua vitalu vya miche inayozalishwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Jiji la Dodoma pamoja na vikundi katika eneo la Mailimbili leo Desemba 21, 2023.
Sehemu ya vya miche inayozalishwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Jiji la Dodoma pamoja na vikundi katika eneo la Mailimbili vilivyokaguliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo, leo Desemba 21, 2023.

By Jamhuri