Rais atangaza elimu bure kwa wanafunzi wa uhandisi na tiba

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuanzia mwaka huu serikali itatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi watakaofanya vuzuri katika mitihani ya kidato cha sita na kuchagua kusomea fani ya Uhandisi na tiba.

Rais Samia ameyasema hayo akiwa mkoani Njombe mara baada yakukagua majengo ya hospitali ya rufaa mkoani humo ambayo ujenzi wake unaelekea ukingoni na kuongeza kuwa wanafunzi hao watafadhiliwa kwa kipindi chote cha masomo yao.

“Wanafunzi watakaofanya vizuri sana! na kuchagua kusomea Uhandisi na Tiba watafadhiliwa masomo yao kwa kipindi chote iwe ni miaka mitano au saba watasoma bure, wao watagharamia chakula na mahitaji yake binafsi” amesema.

Sanjari na hilo pia Rais Samia amesema serikali inafanya jitihada ya kuhakikisha kuwa mpaka kufikia mwaka 2025 nusu ya Tanzania iwe inawaka umeme hivyo hakutakuwa na mkoa ama wilaya itakayokuwa giza.

Amesema serikali itakapofikia hatua hiyo itakuwa imepunguza kazi kubwa na kubakiwa na kazi ndogo ya kufikisha umeme huo kwenye nyumba za watu pamoja na taasisi huku nusu ya maeneo yaliyobaki ikiendelea kumaliziwa taratibu.