Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Mwanza

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 22 yenye thamani ya Bilioni 27 katika sekta ya elimu, barabara,maji,usafi wa mazingira na afya.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 10,2022 na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza Frank Mkilanya, alipokuwa akitoa taarifa ya utendaji kazi wao kwa kipindi cha miezi mitatu kwa waandishi wa habari.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza Frank Mkilanya akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya utendaji kazi wao kwa kipindi cha miezi mitatu kwa waandishi wa habariĀ .

Amesema ufuatiliaji huo ulibaini mapungufu katika miradi ya afya,maji na elimu ikiwemo kuchelewa kukamilishwa kwa miradi hiyo kwa mujibu wa mkataba kutokana na upungufu wa fedha zilizotolewa na Serikali,baadhi ya wazabuni kushindwa kuleta vifaa na vifaa tiba kwa wakati,kupanda kwa bei za vifaa vya ujenzi uliosababisha ongezeko la gharama za ujenzi pamoja na manunuzi kufanyika kwa gharama ya juu ya bei ya soko.

Mkilanya amesema Takukuru inaendelea kushirikiana na wadau ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

Ameongeza kuwa Takukuru katika uzuiaji rushwa imekuwa ikifanya kazi ya uchambuzi wa mifumo ili kubaini maeneo yenye mianya ya rushwa katika utoaji wa huduma kwa Wananchi na kisha kutoa ushauri wa namna bora ya kuziba mianya hiyo.

Ameeleza kuwa wamekuwa wakito elimu kwa umma ili wawe na uelewa wa pamoja wa mambo mbalimbali ya kukemea na kuzuia rushwa katika maeneo yao,na katika kipindi cha April-Juni 2022 Takukuru Mkoa wa Mwanza imetoa elimu kwa makundi mbalimbali kwa kufanya semina 30,mikutano ya hadhara 17 ,uandishi wa makala 11 na maonyesho 2.

By Jamhuri