Wiki iliyopita Rais John Magufuli amefanya
ziara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Moja
ya ziara zilizotugusa ni ziara aliyoifanya
mkoani Mwanza. Akiwa Mwanza amezindua
ujenzi wa meli kubwa yenye uwezo wa
kuchukua abiria 1,200, mizigo tani 400 na
magari 20. Ujenzi wa meli hii mpya
utakwenda sambamba na ukarabati wa meli
za MV Victoria na MV Butiama.
Pia rais amelipa mishahara ya wafanyakazi
waliokaa karibu miaka miwili bila kulipwa
mshahara. Ujenzi wa meli hii ni ukombozi
kwa wakazi wa mikoa wa Kagera, Mwanza
na Mara. Itakumbukwa kuwa Mei 21,
mwaka 1996 meli ya MV Bukoba ilizimika
na kuua watu zaidi ya 1,000.
Tangu wakati huo serikali iliahidi kununua
meli mpya, ila imepita miaka 22 kabla ya
ahadi hiyo kutekelezwa. Meli mpya

inagharimu Sh bilioni 88.7. Meli za MV
Victoria na Butiama zitakarabatiwa kwa
gharama ya Sh bilioni 22.7 na Sh bilioni 4.8.
Pia Serikali itajenga chelezo kwa gharama
ya Sh bilioni 35.9.
Sisi tunasema uamuzi huu ingawa
umechelewa kufanywa na serikali
zilizotangulia, unastahili kupongezwa.
Wakazi wa Kanda ya Ziwa, hasa Mkoa wa
Kagera wamepata tabu sana. Usafiri kwa
wananchi wa Mkoa wa Kagera kwa muda
mrefu umekuwa mgumu. Barabara zilikuwa
hazipitiki kutoka Lusaunga hadi Kahama,
lakini pia pori la Burigi kwa muda mrefu
limekuwa na watekaji.
Ukiacha ukweli kwamba wananchi walikuwa
wanateseka, serikali kwa upande wake
imekuwa ikipata hasara kubwa. Wananchi
walikuwa wanatumia muda mrefu
barabarani kutoka Bukoba kwenda Mwanza
na kinyume chake. Lakini pia serikali
imekuwa ikipata hasara kubwa kutokana na
magari ya mizigo kuharibu barabara.
Usafiri wa majini una faida kubwa. Mzigo
mzito uliokuwa unasafirishwa kwa njia ya

barabara na kuharibu lami ambayo
ingedumu muda mrefu, sasa utasafirishwa
kwa meli. Mbali na kuzipunguzia barabara
mzigo, usafiri wa majini ni wa kasi. Kwamba
wananchi watatumia saa sita kutoka
Mwanza hadi Bukoba ni habari njema.
Ni matumaini yetu kuwa meli hii itafanya
kazi mara mbili kwa siku. Hatutarajii meli hii
itoke Mwanza saa 4 usiku, ifike Bukoba saa
12 asuhubi kama ilivyokuwa MV Victoria,
kisha ishinde pale Bukoba. Meli hizi
zijiendeshe kibiashara. Kama ‘winch’ za
kupakia na kupakua mzigo ndizo shida, hili
liangaliwe.
Tunatarajia meli hizi zikitengamaa zipishane
majini kama boti za Zanzibar. Meli isafiri saa
sita kutoka Mwanza kwenda Bukoba na
ikifika, saa 12 asubuhi ipakue na kupakia
mizigo, kisha saa 6:00 mchana ianze safari
ya kwenda Mwanza, nako ikifika ishushe
mizigo na kupakia, saa 6:00 usiku ianze
tena safari ya Bukoba.
Kwa kufanya hivyo itatoa uhuru kwa
wafanyabiashara wanaotaka kwenda
kununua mzigo na kurejea ndani ya saa 6

au 12 kwa siku. Hii isizuie meli za MV
Butiama na MV Victoria nazo kuongeza kasi
zikafanya kazi kwa muda huo. Utengenezaji
wa meli hizi uende sambamba na
uimarishaji wa usafiri wa treni hadi Mwanza
kutokea Dar es Salaam. Meli ziende
Uganda na Kenya pia. Hongera Rais
Magufuli.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share