Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema mitambo miwili ya kuzalisha umeme kwenye bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), Rufiji mkoani Pwani itawashwa mapema mwakani na kusaidia kuongeza kiwango cha umeme nchini.

Aliyasema hayo jana usiku kwenye ukumbi wa The Super DOM Masaki wakati wa hafla ya kutoa tuzo kwa wenye viwanda waliofanya vizuri iitwayo President Manufacturer of the Year (PMAYA), ambazo huandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI).

Alisema mwezi Januari utawashwa mtambo mmoja kuanza kuzalisha umeme na kisha mwezi wanne utawashwa mtambo mwingine hali itakayosaidia kupatikana umeme wa kutosha na kuondoa malalamiko ya uhaba wa nishati hiyo.

“Ile mitambo iko tisa, sasa kwa kuanzia itawashwa mitambo miwili ambayo itasaidia sana kuongeza kiwango cha umeme hapa nchini na kupunguza malalamiko ya upungufu wa nishati hiyo,” alisema

Alisema ingawa takwimu duniani zinaonyesha kwamba sekta ya viwanda ilidorora miaka miwili iliyopita lakini kwa Tanzania inaonyesha kwamba inakuwa hata kama si kwa kiwango kikubwa.

“Takwimu zinaonyesha tunakwenda vizuri sana kwenye sekta ya viwanda ila kama kuna changamoto sasa ni kuchukua hatua za haraka kuzitatua ili twende kwa kasi zaidi,” amesema.

Aidha, Rais Samia alisema lazima jitihada zifanyike kuondoa utegemezi kwa wenye viwanda nchini kutegemea malighafi kutoka nje ya nchi na badala yake wawe wanatumia malighafi zinazopatikana hapa nchini.

Alisema iwapo viwanda vitaondokana na utegemezi huo vitazalisha bidhaa nyingi na ambazo zitauzwa kwa bei nafuu kwenye masoko ya ndani na yale ya kimataifa hivyo kusaidia kupata fedha za kigeni.

Rais Samia alisema amefurahishwa kusikia kuwa kuna kiwanda cha kuunganisha magari Mkuranga mkoani Pwani ambacho kimekuwa kikitumia malighafi kutoka Tanzania.

Akizungumzia uhaba wa dola za Marekani, Rais Samia alisema kwa Tanzania hali ni nzuri kulinganisha na mataifa ya jirani na aliwaomba wenye viwanda kusaidia kuzalisha bidhaa nyingi na kuuza nje ya nchi ili kupata fedha nyingi za kigeni.

Alisema serikali imeendelea kuongeza kiwango cha wafanyabiashara nchini kutoa Dola za Marekani kwa siku kutoka dola 500, 000 kwa siku hadi kufikia dola 2,00,000 kwa siku.

“Ukilinganisha na wenzetu sisi tuna ahueni kidogo kwasababu tulianza na kikomo cha dola 500,000 kwa siku tukaenda dola 1,000,000 na sasa ni dola 2,000,000 kwa siku sasa kuna majirani zetu hata kutoa dola 500,000 kwa siku hawaruhusu,” alisema

Alisema serikali imechukua hatua kadhaa za kulinda hifadhi ya dola zilizopo nchini ikiwemo kupunguza manunuzi ya bidhaa nje ya nchi na imeingia kwenye kilimo cha mazao ya haraka haraka yatakayouzwa nje ya nchi na kupata fedha za kigeni.

“CTI na wanachama wenu mnaweza kutusaidia sana kupunguza tatizo la uhaba wa dola kwa kuzalisha bidhaa nyingi sana na kuziuza nje ya nchi ili kupata fedha nyingi za kigeni,” alisema Rais Samia

Akizungumzia sukari, Rais Samia alisema kuanzia mwakani Tanzania itaondokana na uhaba wa sukari na itakuwa na uwezo wa kuzalisha ziada itakayokuwa inauzwa nje ya nchi.

Kuhusu malalamiko ya muda mrefu ya wafanyabiashara kutaka gharama za stempu za kielektroniki kushuka bei, Rais alisema linafanyiwa kazi na kuna dalili kwamba gharama zitashuka hivi karibuni.

Katika hatua nyingine, Rais Samia aliwaomba wafanyabiashara na wenye viwanda kuendelea kufanyakazi kwa kufuata sheria za nchi na kulipa kodi kwa hiyari kwasababu serikali imeweka mazingira mazuri na hakuna atakayedaiwa kodi kwa nguvu.

“Wote ni mashahidi hakuna kodi inayodaiwa kwa Defenda siku hizi kwa hiyo ninachowaomba ni nyinyi kulipa kodi kwa hiyari na kufuata sheria za nchi yetu. Ingawa tunakopa kopa lakini mapato ya ndani yanaridhisha na tunamudu kufanya mambo yetu madogo madogo,” alisema

“Ahadi yangu kwenu ni waziri kuwa karibu sana nanyinyi, najua Waziri yuko karibu nanyinyi lakini nataka uwe karibu nao zaidi, chukua changamoto zao zifanyie kazi haraka zisikae muda mrefu kwa sababu nchi imefunguka na huko nje wengi wanatakani kuja,” alisema Rais Samia

Mkurugenzi wa CTI, Leodegar Tenga, alisema tuzo hizo zimekuwa chachu kubwa kwa maendeleo ya viwanda nchini kwani wengi wameongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa umeendelea kuongezeka.

Alitaja vigezo vilivyowezesha kuwapata washindi kuwa ni pamoja na ufanisi katika uzalishaji, mauzo ya nje, uwekezaji katika teknolojia, uwiano wa kijinsia na mchango wa kiwanda katika jamii.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, alisesema wamekubaliana na wenye viwanda wazalishe bidhaa ambazo zitakuwa na uwezo wa kushindana kwenye masomo ya kimataifa.

Dk. Kijaji alisema katika kuhakikisha taifa linanufaika na utekelezaji wa mkataba wa eneo huru la biashara Afrika, tayari wameandaa mkakati wa kitaifa wa utekelezaji wa mikataba huo ambao umeshakamilika na utazindulia mapema Januari mwakani pamoja na kamati ya taifa ya kusimamia utekelezaji wake.

By Jamhuri