Na Wilson Malima JAMHURI MEDIA Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi kuwa na utamaduni wa kutunza kumbukumbu za maisha yao kwa manufaa na mchango kwa vizazi vya sasa na vya baadaye.


Rais Samia ametoa wito huo leo katika uzinduzi wa tovuti ya hifadhi za nyaraka za Dkt. Salim Ahmed Salim (The Dr. Salim Ahmed Salim Digital Archive) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano Cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Septemba 30, 2023.


“Hakika hii ni hazina kubwa kwa taifa letu ina manufaa kwa wale wote wanaopenda kujifunza masuala ya uongozi Diplomasia na Mahusiano ya Kiamataifa.”Amesema Rais Samia


Kwa kutambua, kuthamini ikiwa ni pamoja na kuenzi mchango na jitihada za Dk. Salim katika utumishi wake uliotukuka ndani na nje ya Tanzania hususani katika nyanja ya Diplomasia, Rais Samia amekipa Chuo cha Diplomasia kilichoko Dar es Salaam jina la Dk. Salim Ahmed Salim Center for Foreign Relations.


“Na kwasababu mcheza kwao hutunzwa, na tumesema alikuwa mwanadiplomasia mahiri, tumekubaliana kukipa Chuo kile cha Diplomasia jina na sasa rasmi kitakuwa kinaitwa Dr. Salim Almed Salim Centre for Foreign Relations.” Amesema


Rais Samia amemuelezea Dk.Salim kama Mtanzania na mwanadiplomasia mahiri aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi na bara la afrika kwa ujumla kutokana na utashi wake mkubwa kisiasa na kidiplomasia ambapo katika uongozi wake wakati akiwa balozi wa India na kisha China aliimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo ambayo baadaye yalikuja kuanzisha viwanda vidogovidogo nchini kama vile kiwanda cha Urafiki lakini pia reli ya TAZARA.


Kwa upande mwingine Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Sinde Warioba amemzungumzia Dk.Salim kama kiongozi aliyeweka maslahi ya Taifa mbele na aliyekuwa akipiga vita unaguzi, udini, na ukabila.


Naye Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma ameelezea alichojifunza kwa Dk. Salim katika kuhifadhi kumbukumbu ambapo amesema ni upekee aliokuwa nao jamboa ambalo siyo rahisi kwa viongozi wengine.


“Kitu kikubwa ambacho nimejifunza kwa Dkt Salim ni nidhamu ya uhifadhi wa kumbukumbu maana yake hata sasa hiivi tunafikiria kwa mfano uweke archives za viongozi mbalimbali lakini kupata kumbukumbu kama alivyofanya Dkt. Salim Ahmed Salim itakuwa ngumu sana” amesema Mwinjuma


Vilevile, Mchambuzi wa masuala ya Diplomasia na Uchumi Ayubu Madenge akizungumzia uzinduzi wa hifadhi za nyaraka hizo kidijitali amesema ni wigo mpana umefinguliwa kwa taarifa kuweza kuwafikia wengi pia amewahasa vijana kuiga mfano wa aliyo yafanya Dkt. Salim kwa kukubali kujijenga na kufundishwa pia kupenda kusoma vitabu au machapisho na kuacha visingizio mbalimbali.


“Archive hii ya Dkt.Salim Ahmed Salim, nadhani visingizio vinapungua sasa kwamba upatikanaji wa taarifa zinazomhusu Dk Salim Ahmed Salim zinapatikana, lakini pia mimi niwahase vijana wa wakati wetu kwamba usomaji ni jambo la muhimu sana, wanasema mtu aliyesoma ni mtu aliyeishi maisha mengi sana” amesema Madenge

By Jamhuri