Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Vyuo Vikuu kupitia mitaala yake ili ijikite katika kutoa elimu ambayo inakidhi mahitaji ya jamii.


Rais Samia ametoa wito huo leo mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari (Doctor of Letters -Honoris Causa) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Mahafali ya 52 Duru ya Tano ya Chuo hicho yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City


Aidha, Rais Samia amesema mitaala hiyo itawezesha kutoa elimu ambayo inalenga kutoa wahitimu wenye weledi, wanaoajirika na wajasiriamali.


Rais Samia amesema pamoja na kuwa na uhuru wa kitaaluma, vyuo vikuu vina wajibu wa kutoa mchango wake katika kuleta maendeleo, kutoa elimu stahiki, kufanya tafiti na kutoa maoni ili kulikuza na kuliimarisha taifa letu


Rais Samia pia amesema elimu inayotolewa na taasisi za elimu ya juu inapaswa kuwawezesha wahitimu kujiajiri, kuajiriwa, kuwa wajasiriamali na kuwa tayari kuchangia maendeleo ya taifa letu.
Vile vile, Rais Samia amevitaka vyuo vikuu kuwa na mikakati na malengo yanayolenga kufikia juu zaidi katika mzani wa kimataifa.


Hali kadhalika, Rais Samia amesema Serikali inafuatilia na kutoa mchango kwa kuweka Sera na mikakati ambayo inajumuisha kuendelea kuongeza bajeti ya elimu.

By Jamhuri