Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameanza ziara maalum ya siku nne katika Klabu ya FC Barcelona nchini Hispania kwa mwaliko wa Rais wa klabu hiyo, Joan Laporta.

Makonda ameanza ziara hiyo tarehe 14 Septemba 2026 kwa kufanya mazungumzo na uongozi wa klabu kuhusu fursa za ushirikiano katika maendeleo ya soka nchini Tanzania.

Mazungumzo hayo yalijikita katika maeneo ya kukuza vipaji, maendeleo ya kiufundi, uendeshaji wa timu ya taifa, pamoja na namna uzoefu wa Barcelona unavyoweza kusaidia maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Barcelona inatambulika duniani kwa mfumo wake wa kukuza na kuendeleza vipaji vya wachezaji, jambo linaloifanya kuwa miongoni mwa klabu zinazotumika kama mfano katika maendeleo ya soka la kisasa. Aidha, sehemu kubwa ya wachezaji wa timu ya taifa ya Hispania iliyotwaa Kombe la Dunia 2026 wametokea FC Barcelona.

Katika ziara hiyo, Rais Laporta pia amempatia Makonda salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia kifo cha mume wake, Mzee Hafidh Ameir Hassan, kilichotokea tarehe 7 Septemba 2026.

Laporta amemkabidhi Makonda barua maalum ya rambirambi kwa ajili ya kumfikishia Rais Samia, akimtaka aendelee kuwa na moyo wa subira na ujasiri katika kipindi hicho cha majonzi.

Makonda akiwa ameambatana na Wataalamu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), anatarajiwa kushuhudia mchezo kati ya Barcelona na Racing Santander utakaochezwa tarehe 16 Septemba 2026 katika Uwanja wa Camp Nou, jijini Barcelona, akiwa na mwenyeji wake Joan Laporta, Rais wa FC Barcelona.