Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema maandalizi ya kuupokea ugeni huo yamekamilika ambapo baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Songea ataenda moja kwa moja katika Makumbusho hiyo ya Vita vya MajiMaji.

Amesema akiwa katika Makumbusho hiyo atapata historia ya makumbusho hiyo na kutoa heshima kwa mashujaa waliokufa katika vita hivyo vilivyopiganwa mwaka 1905- 1907.

Kanali Thomas ameongeza kuwa pamoja na kutoa heshima kwa mashujaa wa Vita vya Majimaji, Rais huyo wa Ujerumani atakutana na baadhi ya wahanga wa vita hivyo na kutembelea Shule ya Msingi MajiMaji.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamshna Benard Wakulyamba amesema Wizara ya Maliasili na Makumbusho ya Taifa wanaosimamia Makumbusho ya MajiMaji wamekamilisha maandalizi kwa ajili ya kumpokea Rais huyo wa Ujerumani.

Dkt. Frank-Walter Steinmeier yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia Oktoba 30 hadi Novemba 1, 2023.

Ziara hii mbali na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Ujerumani, pia imelenga kukuza na kuimarisha misingi ya biashara na uwekezaji.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Laban Thomas akizungumzia maandalizi ya kumpokea Rais wa Ujerumani, Mhe. Dkt Frank Walter Steinmeier wakati atakapotembela Makumbusho ya Kumbukumbu ya Vita vya MajiMaji Songea Mkoani Ruvuma, tarehe 1 Novemba 2023
Majadiliano yakiendelea kuhusu mapokezi ya Rais wa Ujerumani, Mhe. Dkt Frank Walter Steinmeier wakati atakapotembela Makumbusho ya Kumbukumbu ya Vita vya MajiMaji Songea Mkoani Ruvuma, tarehe 1 Novemba 2023