Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Taarifa za utafiti wa viashiria na Matokeo ya VVU na Ukimwi Nchini Tanzania kwa Mwaka 2022/2023 zimekamilika huku takwimu za Utafiti huo zikitarajiwa kutolewa rasmi Desemba Mosi Mwaka huu mkoani Morogoro katika maadhimisho ya Siku ya UKimwi Duniani.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 31,2023 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamilika kwa utafiti huo na kueleza kuwa utafiti huo unaonesha Tanzania imepata matokeo chanya kutokana na idadi ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kuendelea kupungua ikilinganishwa na utafiti uliofanywa 2016/2017.
Hatua hiyo inatajwa kuwa ni mafanikio mazuri ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imeyafikia kuelekea kufikia Mlmalengo ya kitaifa ya kufikia SIFURI TATU – yaani lutokuwa na maambukizi mapya, kutokuwa na unyanyapaa na ubaguzi, na lutokuwa na vifo Vitokanavyo na UKIMWI.
Waziri Mhagama ameeleza lengo la utafiti huo kuwa ni kupima mwenendo wa maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi Nchini ikiwa ni pamoja na kuisaidia nchi kuchukua hatua katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi na kujitathimi.
“Lengo la utafiti huu ni kupima matokeo ya juhudi za mapambano dhidi ya UKIMWI, kupitia utafiti huu, tutapata taarifa kuhusu viashiria na matokeo ya VVU/UKIMWI katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka 2022/23 ambazo ni takwimu muhimu kuhusu hali ya UKIMWI nchini, “amefafanua Waziri huyo
Amefafanua kuwa utafiti huo uliokamilika ni utafiti wa tano ambapo nchi hufanya tafiti kila baada ya Miaka mitano ili kujipima katika mapambano dhidi ya Ukimwi ambapo umeshirikisha Wataalam mbalimbali wa Tanzania Bara ,Zanzibar na Wataalam toka nje ya Nchi.
“Kwa taratibu zilizopo huwa tunaanza kutoa taarifa kisha baada ya muda tunatoa matokeo,kwa Serikali yetu huu utafiti si wa kwanza imekuwa ikifanya utafiti kila baada ya miaka Kitano na utafiti wa mwisho ulifanyika 2016/2017 lengo kujaribu kupima matokeo ya juhudi zero ndani ya taifa na kupambana dhidi ya ukimwi, “amesema
Pamoja na hayo ameeleza kuwa,”Utafiti huu umefanywa na Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania kupitia Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI ,Tume ya Kudhibiti UKIMWI Zanzibar, Ofisi ya Taifa ya Takwimu,Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya Serikali zikiwemo Kituo cha Kudhibiti Magonjwa na Kinga na Chuo Kikuu cha Columbia, “amesema
Amewataja Wadau wengine ni Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI na Mpango Jumuishi wa kupambana na UKIMWI, Homa ya Ini, Kifua Kikuu na Ukoma na kufafanua kuwa Kazi hiyo imefanyika kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kudhibiti UKIMWI.
“Natoa wito kwa wananchi kupokea taarifa hii ya awali na kujiandaa kupokea matokeo rasmi ya utafiti huu ifikapo Disemba Mosi, 2023.
Asanteni kwa kunisikiliza, ” amesema.