#Yageukia vyuo vikuu, kati kutengeneza wataalam
#Iko mbioni kurekebisha mitaala kuongeza tija sekta ya madini
#Yadhamiria kutafsiri Vision 2030 kwa vitendo
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali iko mbioni kupitia na kurekebisha mitaala ya elimu kwa vyuo vikuu na vya kati kwa ajili ya kutengeneza wataalam wa kutosha na wenye ushindani mkubwa kuhudumia sekta ya madini nchini.
Hayo yalielezwa na Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Ruben Lekashingo, Oktoba 30, 2023, jijini Dodoma, katika mahojiano maalum na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Madini.
Ameaema katika kutafsiri maono 2030, madini ni maisha na utajiri, Wizara ya Madini imeamua kuongeza nguvu katika nyanja ya uboreshaji wa tija kwa watumishi pamoja na watoa huduma katika sekta ya madini.
Kamishna Janet amesema katika kusimamia ushirikishwaji wa Watanzania katika mnyororo mzima wa Sekta ya Madini, Serikali itashirikiana na kampuni zilizowekeza sekta ya madini hapa nchini ili kujua uhitaji wao kwenye huduma wanazopatiwa na Watanzania katika miradi yao.
“Tunashirikiana na kampuni hizi ili kujua nini wanahitaji, ili tuboreshe mitaala kwenye vyuo vyetu, kuanzia vyuo vikuu hadi vyuo vinavyofundisha wanaotoa huduma, tunataka tuwe na mitaala ya kimataifa ili wakitoka mafunzoni wakatoe huduma stahiki, wapate uzoefu na waelewe kazi kimatendo” amesema Janet.
Aidha, Kamishna Janet amesisitiza kuwa namna nyingine iliyopangwa ni kuwaangalia Watanzania ambao walifanya kazi hapa nchini na kutoka nje kufanya kazi kama wataalam kwa kupata taarifa zao ili warudi nchini kufanya kazi kwenye kampuni zilizopo kwa lengo la kufundisha Watanzania ujuzi waliojifunza katika nchi tofauti tofauti.
Kamishna Janet aliongeza kuwa lengo la wizara kufikia 2030 ni kuhakikisha huduma stahiki inatolewa kwa maboresho ili kuongeza tija kupitia wataalam wa ndani na nje ya nchi kwa watumishi na wafanyakazi kwenda nje kujifunza au kuleta wataalam kuja kuwafundisha wafanyakazi hapa nchini.
“Kwa kuangalia kazi zilizopo na kuangalia huduma tunayotoa kwa wateja wetu, tunahitaji kutoa huduma kwa kiwango gani katika kila kazi iliyopo kwenye muundo wetu, tuongeze nini kwa kuangalia mapungufu yaliyopo ili kuongeza tija, tunahitaji wataalam wazawa wenye uwezo mkubwa na viwango vya kimataifa.” alisisitiza Janet.
Sambamba na hilo, Kamishna Janet alisema njia nyingine ni kuhakikisha kunakuwa na mfumo wa utoaji huduma stahiki kwa kuangilia mataifa yaliyopiga hatua zaidi katika utoaji huduma kwa kuangalia wapi wamefanikiwa zaidi ili kuongeza tija.
Katika kikao Cha Wachimbaji Wakubwa na Wadogo kilichofanyika Oktoba 27, 2023 jijini Dar es Salaam, Kamishna Janet alidokeza mambo kadhaa ambayo Serikali imepanga ikiwa ni maandalizi ya Tanzania kuhakikisha inashiriki ipasavyo katika uchumi wa Madini Mkakati na Muhimu.
VISION 2030: Madini ni Maisha na Utajiri