Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

Serikali imesema inatarajia kuupeleka tena Muswada wa Bima ya Afya kwa wote bungeni Novemba 1,2023 ambao ulikwama Februari mwaka huu baada ya hoja iliyotolewa na Bunge ya kutokuwepo kwa chanzo endelevu cha fedha kutekeleza mpango huo.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Afya Englibert Kayombo ameeleza hayo jana jijini hapa na kwamba Muswada huu ni ndoto ya Serikali ya miaka mingi ambapo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amehakikisha uboreshaji wa huduma bora za afya kuanzia ngazi ya Taifa hadi ya msingi ili wananchi watakapojiunga na nima ya afya waweze kupata huduma karibu na maeneo yao.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya, wadau wa sekta na wataalam wengine tayari wamefanyia kazi hoja zote zilizoibuliwa na Bunge pamoja na wadau, hata hivyo semina elekezi zimefanyika kwa makundi mbalimbali ndani ya jamii kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa wote na maoni yaliyopatikana yalifanyiwa kazi, hivyo wananchi kesho watege macho na masikio yao bungeni kujua nini ambacho Waziri wa Afya Ummy Mwalimu atawasilisha Bungeni.

“Kupitishwa kwa muswada huo kutawezesha kila Mtanzania kuwa ndani ya Mfumo wa bima ya afya hatua itakayoboresha zaidi upatikanaji wa huduma za matibabu bila kuwa na kikwazo cha fedha, ” amesema na kuongeza;

“Serikali yetu ni sikivu na imefanyia kazi hoja zote zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi hivyo yaliyomo ndani ya muswada huo yamelenga kuwasaidia wananchi kupata huduma bora za afya bila ya kikwazo cha fedha”amesema Kayombo.

Kuhusu gharama za vifurushi, Kayombo amesema kuwa mara baada ya Muswada huo kupita na kuwa Sheria, kanuni zitatungwa ili kuratibu suala ya gharama za vifurushi na kusema kuwa uchambuzi utafanyika ili vifurushi viwe vya gharama nafuu na kila mwananchi aweze kuwa na bima ya afya.

Ameongeza kuwa kwa upande wa Serikali imeshakamilisha maandalizi ya kutoa huduma kwa wananchi kupitia mfumo wa bima ya afya kwa wote ambapo imeboresha ubora wa huduma katika vituo vyake vya kutolea huduma ikiwemo upatikanaji wa dawa, ununuzi na usimikaji wa vifaa na vifaa tiba pamoja na ajira za watumishi.

Pamoja na hayo amesema,”kwa sasa nchi yetu iko mbali sana katika utoaji wa huduma, tuna vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa, huduma nyingi za kibingwa zinapatikana hapa nchini lakini pia huduma za afya zimesogezwa sana kwa wananchi hivyo kama nchi tupo tayari kutekeleza hili, nia na uwezo wa kufanya hivyo tunao”amesema.