RC Hapi aongezewa makali

Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Huenda panga pangua ya viongozi mkoani Mara ikaanza kuchukua mkondo wake kwa kasi.

Ni baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuutembelea mkoa huo na kubaini upungufu mwingi, ikiwamo kutelekeza miradi ya maendeleo kwa kipindi kirefu.

Akiwa mkoani humo mwishoni mwa wiki iliyopita, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere inayojengwa Musoma Mjini na kuridhishwa na hatua ya ujenzi ilipofikia.

Katika ziara hiyo amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ali Hapi, kufanyia kazi upungufu uliopo ikiwamo hatua ya kuwawajibisha viongozi wasiowajibika.

“Mkoa wa Mara unaingiziwa fedha nyingi lakini zinafujwa, kuna ucheleweshwaji wa makusudi wa fedha kufikishwa kwenye miradi.

“Suala hili linafanywa makusudi huku viongozi wote mpo. Katika hili nakuagiza mkuu wa mkoa ufanye kazi, umeaminiwa na umepewa mamlaka na Rais, fanya kazi usiogope,” amesema Rais Samia.

Pamoja na agizo hilo kwa mkuu wa Mkoa wa Mara, pia amemtaka Waziri wa Tamisemi ifikapo Februari 18, mwaka huu amfikishie taarifa ya utendaji kazi wa wakurugenzi wote wa halmashauri nchini ili kubaini yupi anafanya kazi na nani hafanyi kazi.

Rais Samia katika ziara hiyo amemuagiza Hapi kuvunja mkataba wa mkandarasi anayejenga barabara ya Makutano ya Juu hadi Sanzate yenye urefu wa kilomita 50. 

Mradi wa barabara hiyo ulianza kutekelezwa tangu mwaka 2013 kwa gharama ya Sh bilioni 54 na milioni 500 lakini hadi sasa haujakamilika.

Mradi mwingine wa barabara ambao Rais Samia amesema mkataba wake uvunjwe ni ujenzi wa barabara ya km 5 ya Musoma hadi Makojo ambayo utekelezaji wake ulianza mwaka 2019 na kutakiwa kukamilika Julai 2020.

Barabara hiyo inayopaswa kujengwa kwa gharama ya Sh bilioni 8.28 mpaka sasa zimeshatumika Sh bilioni 4.5   na hakuna kilometa hata moja iliyokwisha kujengwa. 

Rais Samia amesema kutokana na uwezo mdogo wa kifedha walio nao makandarasi hao mikataba yao ivunjwe na kuanza upya.

Pia Rais Samia ameagiza kusimamishwa kazi wakuu wa idara ya mipango, kitengo cha fedha na wakuu wa idara ya manunuzi wa Halmashauri ya Bunda ili kupisha uchunguzi wa Sh milioni 400 ambazo matumizi yake hayajulikani.

Ziara ya Rais Samia katika eneo yanapojengwa makao makuu ya halmashauri anasema ameshuhudia nondo tu zilizosimikwa.

“Wahusika wanadai vifaa havijasogezwa kwa sababu hakuna ghala la kuhifadhi vifaa, mkandarasi Suma JKT wakati anaanza mradi alitegemea nani amjengee ghala?” amehoji Rais Samia.

Mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 3.5 tayari  Sh bilioni moja zimetolewa na katika fedha hizo kuna Sh milioni 400 hazijulikani matumizi yake.

Pamoja na hujuma hiyo, Rais Samia amesema kuwa kabla ya kuanza kutekelezwa kwa mradi huo kulikuwa na mvutano kati ya majimbo mawili, Jimbo la Mwibala na Jimbo la Bunda, ambapo kila jimbo lilivutia makao makuu ya halmashauri kujengwa kwake.

Rais Samia amesema miradi ya Mkoa wa Mara inakwamishwa na viongozi wa Mara kuwa wabinafsi na kutowajali wananchi wa mkoa huo.

“Viongozi wa Mkoa wa Mara hamko imara – kuanzia wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya hadi mkuu wa mkoa, watu wameiva kwenye wizi tu, watu wa Mara badilikeni,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ambaye ameingia mkoani Mara kwa mambo mawili; kuadhimisha miaka 45 ya kuzaliwa CCM na kufanya ziara ya ndani ya mkoa huo, amesema mwaka 2018 akiwa makamu wa Rais aliitembelea hospitali ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyojengwa tangu miaka ya 1970 na kuona hali yake.

“Nilichukua mapendekezo na kuyafikisha kwa mwenzangu aliyekuwapo, fedha zikatengwa, ujenzi ukaanza mwaka 2019 baada ya kuwa imetelekezwa kwa zaidi ya miaka 40,” amesema Rais Samia na kuahidi kuwa hospitali hiyo ikikamilika itakuwa na kitengo maalumu cha kibingwa cha kuhudumia masuala ya ajali na mifupa.

“Nikiwa bungeni nilikuwa nakaa jirani na Gaudencia Kabaka, nilikuwa namuona yeye pamoja na wabunge wenzake wakisaka fedha, siku moja nikamuuliza ni fedha ya nini?

“Alinionyesha picha za watu waliopigana mapanga na kukatana mifupa iko nje, wengine wamekatana kwenye bega na wengine vichwa vimepasuka, akaniambia ni fedha ya kujenga hospitali ya kushughulikia mambo hayo,” amesema Rais Samia.

Katika ziara hiyo, Rais Samia ametembelea Musoma Vijijini na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji utakaonufaisha wananchi 164,000 wa eneo la Musoma Vijijini hadi Butiama. 

Mradi huo unagharimu Sh bilioni 70 na hadi sasa asilimia 75 ya fedha zote imekwisha kutolewa.

Rais Samia amewataka viongozi wote mkoani humo na nchini kwa ujumla sifa wanazozitoa kwenye ujenzi wa madarasa nchi nzima wazihamishiwe kwenye ujenzi wa vituo vya afya na miradi ya maji inayotekelezwa nchi nzima.