Na Bryceson Mathias, JamhuriMedia, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amekabidhi misaada mbalimbali yenye Thamani ya zaidi ya Shilingi Mil. 27 kwa wakazi walioathiriwa na maafa yaliyotokana na mafuriko yaliyosababisha maporomoko ya tope katika mlima Hanang kata ya Katesh Wilayani Hanang mkoani Manyara.
Misaada hiyo imehusisha vyakula, vifaa mbalimbali pamoja na Fedha Taslim kutoka kwenye Taasisi za Serikali na binafsi pamoja na wahisani walioguswa na maafa hayo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo, mkuu huyo wa mkoa amesema sambamba na kukabidhi misaada hiyo amefika wilayani humo kutoa pole kwa uongozi wa Serikali, majeruhi pamoja na kuwafariji waliopoteza ndugu na mali zao.
Akipokea misaada hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mkuu wa Wilaya ya Hanang Janeth Mayanja amesema Serikali kwa kushirikiana na wahisani imeendelea kuwahudumia walioathirika na janga hilo kwa kuwapatia malazi, matibabu na chakula.
Amesema wakazi wa Kigoma kupitia Mkuu wa Mkoa wamemuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu kwani misaada iliyotolewa itaendelea kuwanufaisha waathirika wa mafuriko hayo ambao kwa sasa wanauhitaji mkubwa wa misaada ya kiutu ili waweze kumudu gharama za maisha.
“Misaada hii mngeweza kuifikisha hata kwa kuituma lakini mmeguswa na mkaona sambamba na kutusaidia mje mtupe pole, hili ni jambo jema hivyo umoja na mshikamano huu uendelee baina yetu zinapotokea changamoto kama hizi” amesema Mayanja.
Aidha Mkuuu huyo wa wilaya ya Hanang ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa misaada iliyotolewa itawafikia walengwa na hakuna mamluki watakaoweza kujiingiza ili kujinufaisha.
Mayanja amesema serikali ilishafanya sensa na kuwajua walioathirika kwa kuwaorodhesha na tayari imewekwa utaratibu maalum wa ugawaji wa misaada kwa watu husika na takwimu zinatunzwa kwa ajili ya ulinganifu wa misaada iliyopokelewa, iliyotolewa na iliyobaki katika maghala ili kuziba mianya ya udanganyifu katika misaada hiyo.