Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Rufiji

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji ,kuandaa mipango na bajeti kwa kuzingatia vipaombele vinavyolenga kuwandolea wananchi kero na kuwainua kimaendeleo.

Maagizo hayo ameyatoa kwenye kikao maalum cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichoketi Juni 19 mwaka huu ,kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali – CAG kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo wilaya hiyo imepata hati safi.

Aidha amesema, hakuna sababu ya halmashauri kuzalisha hoja za ukaguzi iwapo utekelezaji wa shughuli mbalimbali utazingatia na kufuata taratibu zote kwa mujibu wa mipango na bajeti .

Vilevile ameelekeza, kuhakikisha kuwa hoja zote 38 kati 62 zilizopitiwa na kutolewa dosari na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali CAG mwaka wa fedha 2021/2022 zinapatiwa majibu kwa haraka ili ziweze kufungwa.

“Hakikisheni hoja hizi 38 ambazo bado hamjazijibu ikiwa ni pamoja na ya ukusanyaji mapato na uhaba wa wakaguzi wa ndani mnazitolea maelezo haraka ili kupata ufumbuzi wa masuala ambayo yanakwamisha utekelezaji wa shughuli za kuwaletea wananchi maendeleo,“ ameeleza Kunenge.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta aliwashauri viongozi wa Wilaya hiyo kujipanga, kuhakiki ,kuandaa nyaraka na kuzitafutia majibu hoja zote kabla ya mwezi Desemba mwaka huu ili kurahisisha zoezi la ukaguzi wa CAG.

Awali akiwasilisha ripoti ya CAG, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji ,Michael Gwimile aliahidi, kushughulikia dosari zote zilizobainika kwenye ripoti hiyo.

Mkaguzi Mkuu wa nje kutoka ofisi ya CAG Mkoa wa Pwani Mary Dibogo aliishauri Halmashauri hiyo kuongeza idadi ya wakaguzi wa ndani kwa ajili ya kushughulikia na kudhibiti mapema dosari ambazo zinaweza kubainishwa na CAG.

By Jamhuri