Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Simiyu

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda ametoa siku tano kwa Mkuu wa Wilaya ya Busega, Faidha Salim pamoja na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Michael Kachoma kuhakikisha jenereta ya Hospitali ya Wilaya ya Busega mkoani humo inaanza kutumika, ili kusaidia huduma za upasuaji kwa wajawazito, watoto na watu wengine.

Agizo hilo la Dk Nawanda limekuja baada ya kufanya ziara ya kushtukiza hospitalini hapo jana na kubaini jenereta lilitolewa na Wizara ya Afya halijatumika kwa zaidi ya mwaka mmoja, kwa kilichoelezwa kukosekana vifaa vya majaribio ikiwemo, kilo tano za chumvi, makopo mawili ya mkaa, pamoja na lita 15 za mafuta ya dizeli na nyaya mbalimbali.

Ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu
“Natoa siku tano, kuanzia leo Mei 20 hadi 25, 2024 nikute hili jerereta linafanya kazi, kama mtashindwa Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya mtakuwa hamstahili kufanya kazi hapa Busega,” amesema Dk Nawanda na kuongeza kuwa jenereta hiyo itakuwa msaada mkubwa ikiwa umeme utakatika.

Kwa mujibu wa Nawanda, awali watalaamu waliwasilisha bajeti ya zaidi ya Sh milioni 20 kwa ajili ya kununua vitu vyote vinavyohitajika katika majaribio ya jenereta hilo.

“Baadaye ikapungua hadi Sh milioni 18, alipokuja mkurugenzi mpya ikapungua hadi Milioni nne, lakini taarifa zilizopo inaweza kupungua hadi laki nne,” amesema Dk Nawanda.

By Jamhuri