Wananchi wa Kata za Ruhembe, Kidodi, Uwembe, Vidunda, Mikumi na Kilolo waliokuwa wakiteseka kwa muda mrefu kusafiri umbali mrefu au kuzunguka kwenye mashamba ya miwa kuzifikia huduma za kijamii kwa sasa wanaondokana na adha hiyo baada ya serikali kujenga daraja madhubuti kiunganishi cha barabara katika kata hizo.

Mbunge wa Jimbo la Mikumi, wilayani Kilosa, Denis Londo amesema hayo wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa alipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo.

Londo amesema wananchi hao walitumia gharama kubwa katika kuzalisha mazao yao na hali hiyo ilitokana na kukosekana kwa kiunganishi madhuhuti cha miundombu ya barabara katika kata hizo.

Mbunge wa Jimbo hilo amesema  kukosekana  kwa daraja, kulichangia gharama kubwa ya uzalishaji wa mazao kwa mkulima kutokana na kuwapo ugumu wa upatikanaji wa mbegu ,  pembejeo na usafirishaji.

“Hadi mkulima anakuja kuuza mazao yake hapati faida kwa kuwa ametumia gharama kubwa wakati wa kupanda na kukuza mazao yake kutokana na kukosekana kwa miundombinu rafiki” amesema  Londo.

By Jamhuri