Ripoti:Kulikuwa na uzembe wa marubani ajali ya ndege ya Precision

Ripoti ya pili ya ajali ya Ndege ya Precision Air iliyotokea tarehe 6 Novemba ,mwaka 2022 katika Ziwa Victoria, Bukoba, Mkoa wa Kagera na kusababisha vifo vya watu 19 na wengine 24 kuokolewa imeseka kuwa kulikuwa na uzembe wa marubani.

Ndege ya Precision Air iliyokuwa inatoka Dar es Salaam kwenda Bukoba ilikuwa na watu 43 kati yao, 39 abiria, marubani wawili na wahudumu wawili.

Ripoti ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air, ilitoka mwishoni mwa mwezi Novemba, 2022, na ilibainisha kuwa kulikuwa na ucheleweshwaji katika uokozi kwa jeshi la Wana maji kuchelewa kufika katika eneo la tukio.

Ripoti hiyo imeelezea kuwa marubani wa ndege hawakuwa na tatizo la kiafya, ndege ilikuwa imeandikishwa kihalali, hali ya hewa ya katika uwanja wa Bukoba haikuwa nzuri, hali mbaya ya hewa iliathiri marubani kutekeleza jukumu lao.

Pia ripoti hiyo imeeleza kuwa marubani hawakuwa makini katika kufuata ishara za tahadhari zilizotolewa, ndege iligonga kwanza bawa lake la kushoto wakati ikianguka, pia ilianguka kwa kasi na kugonga sehemu ya mbele kwenye kina cha maji ya ziwa Victoria na vifaa vyote vya kuongozea ndege vilikuwa vinafanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya rubani.