Na Immaculate Makilika , JamhuriMedia, MAELEZO

Serikali imesema kuwa imejipanga kuhakikisha sayansi na teknolojia inatumika ili kuleta chachu katika maendeleo nchini.

Akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari leo Jijini Dar es Salaam, kuhusu Kongamano la Kitaifa la Nane la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt Amos Nungu amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwaleta pamoja wadau ambao ni Serikali, wabunifu, watafiti na wananchi pamoja na kutoa fursa mbalimbali zitakazo wanufaisha wadau hao.

“Kupitia Kongamano hili tunatoa fursa kwa wadau wetu ya kukutana, kuhabarishana, kujifunza na kuendeleza shughuli zao”, ameeleza Dkt. Nungu.

Aidha, Dkt. Nungu amesema kuwa Kongamano hilo litakalofanyika Juni 14 – 16, 2023, Jijini Dar es salaam litahudhuriwa na washiriki 500 kutoka ndani na nje ya nchi ambapo pia kutakuwa na mada mbalimbali zinazolenga kuangalia mfumo wa sayansi pamoja na ubunifu na mchango wake katika uchumi.

Ametaja baadhi ya mada kuwa ni uchumi wa kijani, sayansi huria, ubunifu wa maendeleo ya watu na mchango wa maarifa asilia.

Naye, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Uhusiano na Mawasiliano kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Slivia Lupembe alisema kuwa Serikali kupitia Wizara yake imejipanga kuhakikisha sayansi na teknolojia inakuwa chachu ya maendeleo na ndio maana imeendelea kufadhili kazi mbalimbali za kibunifu sambamba na kurasimisha kazi zao ikiwa ni pamoja na kuwasajili ili kuwatambua rasmi.

By Jamhuri