Senyamule aagiza Chemba kujipanga upya

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi katika Kijiji cha Magungu, Kata ya Mpendo, Wilaya ya Chemba na kukemea vikali uongozi wa Kijiji kukusanya fedha kwa wananchi bila kufuata utaratibu.

Senyamule ameyasema hayo jana mara baada ya kufanya ziara yakukagua utekelezaji wa miradi ya boost katika Wilaya ya Chemba.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akikagua ujenzi wa madarasa ya Shule ya msingi Birise unaotekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Boost alipofanya ziara ya kikazi wilayani Chemba leo tarehe 13/06/2023.

“Sijaona dhamira ya dhati katika ukamilishaji wa mradi huu kwa muda tuliokubaliana wa tarehe 30/6/2023, tumekubaliana sote kuwa miradi hii ikamilike kwa wakati lakini leo nimesikitishwa sana hatua hii ya ujenzi ambao uko katika hatua za awali” Senyamule amefafanua.

Alisema hayuko tayari kuona dhamira njema ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea wananchi maendeleo hususan katika nyanja ya elimu haifikiwi kutokana na watu wachache kutotimiza wajibu wao.

“Katika mradi huu Chemba hamjafika hata asilimia 20 na mna siku 18 zimesalia, fedha zilitolewa kwa wakati mmoja nchi nzima, Wilaya nyingine za Mkoa wa Dodoma wako katika hatua za upauji, siko tayati kumuangusha Mhe. Rais, ujenzi ufanyike mchana na usiku” ameagiza..

Katika hatua nyingine Senyamule alikemea vikali utaratibu unaotumiwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Magungu Bw. Bernard Kapaya kuchangisha fedha wananchi bila kibali cha Mkuu wa Wilaya.

“Naomba kuwakumbusha kuwa Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya, vyumba vya madarasa ya awali na msingi, nyumba za walimu na ujenzi wa Vyoo. Wananchi wasishurutishwe kuchangia fedha, wachangie kwa hiari yao wenyewe na utaratibu ufuatwe ikiwa ni pamoja na kuambatanisha muhtasari wa mkutano wa Serikali ya Kijiji na barua iliyopitishwa kwa Mkurugenzi kwenda kwa Mkuu wa Wilaya. Ni kinyume kuchangisha fedha bila kufuata utaratibu huo” ameoonya

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chemba Gerald Mongella amesema kumekuwa na ucheweshaji kutokana na kusuasua kwa mchango wa nguvu za wananchi hali iliyopelekea ucheleweshaji wa upatikanaji wa madini.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule akiongea na Wananchi waliojitokeza kushiriki na kusaidia kazi mbalimbali katika Utekelezaji wa  ujenzi wa mradi wa vyumba vinne (4) vya madarasa ya Shule ya Msingi Birise leo tarehe 13/06/2023 alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua miradi inayoyotekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Boost.

Mkoa wa Dodoma kupitia mradi wa Boost umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 10.6 kwa ajili ujenzi wa Shule mpya 16, vyumba vya madarasa ya msingi 163, madarasa ya awali 16, ujenzi wa vyoo 106, nyumba za walimu 03 na darasa 01 la elimu maalumu. Wilaya ya Chemba imepokea kiasi cha shilingi Bilioni 1.3.

Katika ziara yake Senyamule amekagua maendeleo ya ujenzi wa Shule mpya ya Magungu, Ujenzi madarasa katika Shule ya Msingi Birise, ujenzi wa madarasa Lahoda na Ujenzi wa shule mpya Handa ‘B’.

Maendeleo ya ujenzi wa Madarasa ya Shule ya Msingi Magungu, Shule ya Msingi Birise, Shule ya Msingi Lahoda na Shule ya Msingi Handa ‘B’ yanayoyojengwa wilayani Chemba kupitia fedha za mradi wa Boost.