Na Dotto Kwilasa, JakhuriMedia, Dodoma

OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kupitia Wadau wa Utalii imejipanga kuiweka Dodoma kwenye ramani ya utalii kupitia mkakati wake wa miaka 10 wa kuipeleka Dodoma kwenye soko la utalii la kimataifa ili kuiongezea Serikali mapato.

Hayo yameelezwa Jijini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule kwenye mkutano wake na wadau wa Utalii uliolenga kutafuta mkakati zaidi wa kuimarisha hali ya utalii ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kutangaza vivutio vya utalii na kuweka kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Akizungumza kwenye mkutano huo amesema, Utalii ni mapinduzi ya kiuchumi hivyo kama Mkoa wanahitaji kujiimarisha zaidi kwa kubaini na kuweka alama kwenye maeneo yote ya hifadhi za kihistoria katika Mkoa ili kuvutia idadi ya watu kuja kuwekeza Dodoma.

Senyamule amesema japo mambo hayajawa sawa hatua nyingine zinapaswa kuanza wakati wakiendelea kuimarisha hatua kwa hatua na kushauri kuwepo na ari ya kuhamasisha wafanyabiashara kuwekeza kwenye kumbi za starehe,michezo na kilimo.

“Hatua ya kwanza lazima tutengeneze mkakati zaidi ili kufanikiwa katika hiliDodoma, kwa sasa tumeifikia silimia 50 ya safari ya kuendeleza utalii Dodoma,natoa wito kwa Vyuo vikuu kuongeza mchango wa kuhamasisha utalii, nawashuku UDOM tayari wameanza, ” amesema

Kuhusu utambulisho wa Dodoma,Mkuu huyo wa Mkoa amefafanua,”Nimekuwa nikiulizwa sana kuhusu Icon ya Dodoma, niwaambie tu kuwa mkoa wetu ni wa kipekee tuna vitu vingi vya kututambulisha na kutufanya tuwe na vivutio vya kipelee, mfano zabibu, mji wa kiserikali na Bunge,”amefafanua.

Hata hivyo ameeleza kuwa Serikali inao mpango wa kujenga mnara mrefu wa kuitambulisha Tanzania kutokea Dodoma utakaokuwa na mita 110 ambapo tayari hatua za awali zimeanza na kusisitiza kuwa dhamira ya kuijenga Dodoma ni kubwa.

Kwa upande wake mdau wa Utalii kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM) Prof. Winiester Anderson amesema wao kama wadau wakubwa wa Utalii wameandaa mkakati wa miaka 10 kuileta Dodoma kwenye soko la utalii kwa kubainisha maeneo ya kuvutia watalii na kuiongezea serikali kipato.

Amesena kupitia filamu ya Royal tour tayari Utalii kwa Tanzania unazungumzwa kama ajira na kutizamwa kama sekta inayochangia asilimia mbili ya pato la taifa na kwamba kwa umuhimu huo tayari wameanza kubaini na kuimarisha maeneo ya utalii kwenye maeneo yote ya hifadhi za kihistoria ili kuweka kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Akitolea mfano wa vivutio ametaja eneo lililobeba asili ya neno Dodoma ambalo Tembo alididimia na kuzama moja kwa moja na kupelekea wenyeji na wakazi wa eneo hilo lililopo Kata ya Kikuyu kukiita kitendo hicho Idodomya yaani imedidimia na kupelekea Mkoa huo kuitwa Dodoma hadi leo.

Aliongeza kuwa,watanzania tangu enzi za mababu wamekuwa wakifundwa na kusisitizwa kuipenda asili yao na kuijua kwa kina hivyo ni wajibu wao kuwa vinara wa kutunza asili ya utanzania na kuisemea pale wanapoona mambo yanaharibika ili vizazi vijavyo vifaidi na kuijua asili yao.

Naye Dk. Aman David amesema Mkoa wa Dodoma una vivutio vingi vya kihistoria ambavyo vikiboreshwa vitakuwa na hadhi na kuvutia watalii na kutaja baadhi ya vivutio vya Wilaya ya Bahi kuwa na utalii wa picha kwenye maeneo ya asili kutokana na mandhali yake na kwa Wilaya ya Chamwino maeneo ya utalii ni Ikulu ambapo amesema kuna ile ya zamani na mpya , bwawa la Mtera na ngoma za asili.

“Vivutio ni vingi lakini ,kwa upande wa vile vya asili utambuzi wake umesahaulika mfano Kikuyu mbali na kuwepo kwa eneo la tembo,ukiingia ndani ya chuo kikuu cha St.Jonh kuna mti mkubwa uliotumika kunyongea wahalifu kipindi cha utumwa lakini ukiwauliza wanaosoma pale hawajui chochote kuhusu mti huo,”amesema

By Jamhuri