Wananchi wa kata za Maretadu na Maghang Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, wameishukuru Serikali kwa kuanza ujenzi wa Daraja la Maretadu-Garkawe wakisema kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha mawasiliano na usafirishaji.

Wakizungumza kwenye ziara ya mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga kukagua ujenzi wa daraja hilo la mawe linalounganisha Vijiji hivyo, wameeleza kuwa mradi huo ni hitaji la muda mrefu katika vijiji vya kata hizo ili kuongeza ufanisi katika huduma za kijamii na kukuza uchumi.

“Nashukuru sana kuhusu daraja letu, tulikuwa tunalia sana hasa hasa sisi wanawake, watoto wa shule, tunaenda hata wakati mwingine kujifungulia nyumbani kwa sababu hakuna namna ya kufika kwenye huduma za afya’ tunamshuru sana Mbunge wetu kwa kututetea” alizungumza Maria Lohay mkazi wa Maretadu.

Meneja wa Wakala wa barabara mjini na Vijijini (RUWASA) wilaya ya Mbulu Mhandisi Nuru Hondo, amesema gharama za Ujenzi wa Daraja hilo la mawe na kufungua barabara kilomita 9.5 ni shilingi Milioni 470,950,000.00.

Amesema mradi huo ulianza kutekeleza Septemba 4/2023 na unategemea kukamilika Aprili 4/2024 ambapo kwa sasa upo kwenye hatua ya Msingi sawa na asilimia 25 ya utekelezaji.

Mbunge wa Jimbo la Mbulu Flatei Massay amesema Daraja hilo halikuwa kwenye bajeti ya mwaka huu ila serikali kwa kujali wananchi wake imeoma ni Muhimu huduma za maeneo hayo ipatikane bila kikwazo cha ukisoefu wa daraja.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga amesema serikali ipo kazini na kwamba barabara zote zisizopitika katika mkoa huo zinafanyiwa ukarabati.

Amesema baada ya Daraja hilo kukamilika fursa mbalimbali zitapatikana ikiwemo wakulima kuuza mazao yao bila kikwazo.

By Jamhuri