Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Serikali imewaagiza wananchi takriban 5,000 waliovamia Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo( RAZABA) ,kuondoka mara moja katika eneo hilo na kuikabidhi Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzania TFS kulisimamia.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alipofika katika eneo hilo na kuzungumza na wakazi wa Kata ya Makurunge iliyopo wilaya ya Bagamoyo .

Amesema maamuzi ya kuwaondoa wananchi hao yametokana na serikali kushughulikia migogoro ya ardhi ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda timu ya Mawaziri wanane wa kisekta iliyoshirikiana na timu ya wataalam na kufika katika maeneno mbalimbali likiwemo la RAZABA na kutoa mapendekezo ambayo yaliridhiwa na baraza la Mawaziri kwa utekelezaji.

Amesema Shamba hilo lilikuwa ranchi ya Mifugo ambayo ilitolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, eneo hili lilikuwa na ukubwa wa hekari 28,097 ambazo ziligawanywa katika shamba namba 364,365/1 na 365/2 Makurunge.

“ Naagiza wananchi wa eneo hili la RAZABA kuondoka mara moja kwa sababu ni mali ya serikali na kuanzia sasa lipo chini ya usimamizi wa Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzania TFS,” anaeleza Kunenge.

Vilevile Kunenge ameagiza leseni ya kampuni ya Sea Salt kupunguza eneo la hekari 50 kati ya 2,000 zinazomilikiwa na kampuni hiyo ambalo litagawiwa kwa ajili ya wananchi wa Kajanjo.

Katika hatua nyingine, amemuagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi, kufuta hati ya upimaji eneo la Mji Mkongwe, uliofanyika ndani ya eneo la hifadhi kwa kuwa zilitolewa ndani ya GN namba 1983 na kutatua mgogoro wa ardhi eneo la magofu ya Kaole na Familia ya Omary Sherdel.

By Jamhuri