Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Biharamulo

KATIKA kuhakikisha taasisi za Umma nchini zinakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia duniani kwa lengo la kurahisisha na kuboresha kazi,halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera imenunua vishikwambi 38 kwaajili ya kuepuka gharama za kutumia karatasi kwenye vikao vya mabaraza ya madiwani.

Uamuzi wa halmashauri hiyo umeonekana kukata kiu ya muda mrefu kwa madiwani wake ambao walikuwa wakilalamikia matumizi makubwa ya karatasi kwenye kabrasha za vikao vyao vya kikanuni, jambo lililokuwa likisababisha baadhi yao kutoishauri vyema halmashauri hiyo.

Akikabidhi kwa madiwani 23 wa halmashauri hiyo, Mkuu wa wilaya ya Biharamulo, Acp Advera Bulimba, ameipongeza halmashauri kwa kutenga fedha za makusanyo ya ndani na kufanikisha ununuzi wa vishikwambi 38 kati ya 45 vinavyohitajika kwaajili ya kukidhi haja ya madiwani pamoja na wakuu wa idara na vitengo.

Kushoto Mkuu wa wilaya ya Biharamulo,ACP. Advera Bulimba,akikabidhi kishikwambi kwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,Leo Rushahu,(kulia)

Aidha Bulimba amewataka madiwani hao kuvitunza na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatunza siri za serikali ambazo zitatumwa kwao kupitia huduma mtandao.

“Kwa kweli nitumie fursa hii kuwapongeza sana halmashauri na madiwani wote kwa kuamua kutoka kwenye uendeshaji baraza kizamani na kuingia katika mfumo wa kidijitali…hili ni jambo muhimu sana isipokuwa mvitunze na kuvitumia kwa malengo kusudiwa” amesema Bulimba.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu, amesema kununuliwa kwa vishikwambi hivyo itasaidia kupunguza gharama zilizokuwa zikiingiwa na halmashauri hiyo kwa kutumia karatasi nyingi,kulipa posho ya msambazaji wa kabrasha za vikao vya madiwani pamoja na mafuta ya magari.

Madiwani wa halmashauri ya Biharamulo,wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa vishikwambi.

“Tunaamini vishikwambi hivi vitaokoa gharama kubwa zilizokuwa zinatumika zamani na kwamba sasa tutaendesha vikao vyetu kidijitali kwa madiwani kupata taarifa za vikao vyetu wakiwa nyumbani badala ya kusubiri kuletewa kabrasha” amesema Rushahu.

Awali Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Inocent Mkandara,amesema kuwa halmashauri hiyo imenunua vishikwambia 38 kati ya 45 ambavyo vinahitajika kwa madiwani pamoja na wakuu wa idara na vitengo na kwamba kila kishikwambi kimegharimu kiasi cha shilingi 600,000.

Hata hivyo amesema madiwani na watendaji hao wamegawiwa kwa kukopeshwa bila riba ambapo kila mhusika ataendelea kulipa fedha kiidogo kidogo na atakapomaliza malipo itakuwa mali yake binafsi.

Kushoto ni Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Biharamulo, Mihayo Miganyalo,akipokea kishikwambi kutoka kwa mkuu wa wilaya hiyo,ACP. Advera Bulimba.

By Jamhuri