Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amezitaka Jumuiya ya Kimataifa na Washirika wa Maendeleo kusaidia mchakato wa kuwarudisha wakimbizi wa Burundi kwa hiari nchini kwao kwa kuweka sawa mazingira ya ndani ya nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia), akisikiliza mada zilizokuwa zinawasilishwa na viongozi wa nchi mbalimbali katika Kikao cha 73 cha Kamati Tendaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wakimbizi (UNHCR), kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Umoja wa Mataifa, jijini Geneva, nchini Uswisi, leo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma kwa Wakimbizi, Sudi Mwakibasi. Nyuma ya Mkurugenzi ni Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania nchini Uswisi, Hoyce Temu. 

Akizungumza katika kikao cha 73 cha Kamati Tendaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wakimbizi (UNHCR), alipokuwa anawasilisha taarifa ya Serikali katika Kikao hicho, jijini Geneva nchini Uswisi, leo, Waziri Masauni amesema Serikali ya Burundi, Tanzania na UNHCR kupitia kikao cha Pande Tatu, walikubaliana ili kuwarejesha wakimbizi hao nchini kwao lazima hali ya mazingira ya ndani ya Burundi yaweze kuwa sawa.

Masauni ameongeza kuwa Burundi kwasasa ina amani na wakimbizi hao waliopo katika Kambi ya Nyarugusu na Nduta Mkoani Kigoma waweze kurudishwa kwao kwa hiari hivyo Jumuiya ya Kimataifa Washirika wa Maendeleo wanaweza kufanikisha mchakato huo kwa kuisaidia Burundi ili wakimbizi hao waweze kurudi katika nchi yao.

“Ili mpango huu ufanikiwe ni lazima hali ya mazingira ndani ya Burundi yaweze kuwa sawa, ili wakimbizi hao wanapoenda wasiweze kurudi nchini, kwahiyo tumewaomba shirika la kimaitaifa pamoja na washirika wa maendeleo kuisaidia Serikali ya Burundi kuhakikisha kwanza wanaweka mazingira mazuri kwa raia wa Burundi kurejea nchini kwao na kuendelea kubakia kule, na pia waendelea kusaidia huduma za wakimbizi katika nchi yetu,” amesema Masauni.

Aidha, Waziri Masauni ametoa pongezi Kamishina Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi kwa kuteuliwa kwa mara nyingine katika nafasi hiyo katika kipindi kingine cha miaka miwili na nusu.

Kikao hicho cha siku tano kilichoanza Oktoba 10, 2022 kinaendelea jijini Geneva ambapo wawakilishi kutoka nchi mbalimbali duniani wanaendelea kuwasilisha taarifa za wakimbizi na kujadiliwa na washiriki wa kikao hicho.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wapili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, nchini Uswisi, Maimuna Tarishi (wapili kulia), Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu nchini humo, Hoyce Temu (kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi, Sudi Mwakibasi, nje ya Ukumbi wa Mikutano wa Umoja wa Mataifa, jijini Geneva, nchini Uswisi, leo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

By Jamhuri