Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amezipiga marufuku kampuni na watu wanazojihusisha na uuzaji holela wa viwanja ambao hauzingatii matakwa ya Sheria ya Mipangomiji Na 8 ya Mwaka 2007 Sura 355.

Ni kampuni za uwakala wa ardhi ambazo zimekuwa zikijihusisha kugawa na kuuza viwanja ambavyo havijapangwa wala kupimwa kwa jina maarufu la 20 kwa 20.

Dkt.Mabula ameyabainisha hayo leo Septemba 1, 2022 wakati akifungua mkutano wa wadau wa uendelezaji milki nchini unaofanyika jijini Dar es Salaam.

“Siku za karibuni kutokana na thamani ya ardhi kupanda,kuwepo kwa hitaji kubwa la makazi na uwepo wa makampuni binafsi ya upangaji, upimaji na makampuni mengine yanayojihusisha na masuala ya ardhi kumetokea wimbi kubwa la uuzaji holela wa viwanja ambavyo havizingatii matakwa ya Sheria ya Mipangomiji kwa baadhi ya makampuni ya uwakala wa ardhi kugawa na kuuza viwanja ambavyo havijapangwa wala kupimwa kwa jina maarufu 20 kwa
20.

“Aidha, hivi karibuni wizara imekuwa ikipokea maombi kutoka kwa wananchi ya kutaka kupimiwa maeneo yao ambayo wanadai kuuziwa na baadhi ya makampuni yakiwa hayajapangwa wala kupimwa.

“Makampuni hayo yananunua maeneo na kukata viwanja vidogo vidogo vyenye ukubwa chini ya mita za mraba 300 bila kuzingatia sheria na mahitaji ya huduma za jamii katika maeneo hayo na kisha kuuza kwa wananchi.

“Maeneo hayo barabara hazifiki upana wa mita nne. Baada ya kuwauzia wananchi wanawaelekeza kufika wizarani kwa ajili ya kupimiwa. Wakati huo wameshauza na kuleta migogoro ya matumizi ya ardhi.Kampuni hizo tumeshazibaini tunaangalia namna ya kuzichukulia hatua kwa mujibu wa sheria,”alibainisha Waziri Dkt.Mabula.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Mipangomiji Na 8 ya Mwaka 2007 Sura 355, Kifungu Na. 77 (1) ((b)), ((i)), Kanuni za viwango vya upangaji wa maeneo zilizotangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na 91 na 93 la tarehe 9/03/2018, ukubwa wa maeneo kwa matumizi mbalimbali umeainishwa.

Aidha, kwa mujibu wa sheria hiyo na taaluma ya mipangomiji, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, viwanja vya matumizi mbalimbali vinatakiwa kuwa na ujazo wa aina mbalimbali kama ujazo wa juu (high density), ujazo wa kati (medium density) na ujazo wa chini (low density) ambapo viwanja hivyo vinatakiwa kuwa na mapana na marefu yenye uwiano wa 1:2 mpaka 1:2.5.

“Kwa mfano, kiwanja chenye ukubwa wa mita za mraba 400 kinapaswa kuwa katika uwiano wa upana wa mita 16 na urefu wa mita 25, uwiano wa 1:1 yaani 20 kwa 20 haukubaliki kitaalam na hakuna kiwanja chenye upana na urefu ulio sawa,”alisema Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Hata hivyo,Waziri Dkt.Mabula alisema,taaluma ya mipangomiji inaelekeza pia kuwa mpangilio wa viwanja kuhusiana na ujazo (density) unategemea mambo mengi ikiwemo umbali kutoka barabara kubwa, umbali kutoka eneo la maji (bahari, ziwa, mto), milima na mabonde.

“Mambo haya yote hayazingatiwi kwenye soko huria la uuzaji wa vipande vya ardhi, na jambo hili limeleta kero kubwa kwa jamii pamoja na kuathiri madhari au muonekano wa miji yetu. Kwa kuwa miji yetu inatakiwa kuwa na maendeleo endelevu ikiwemo makazi na sehemu zingine za jamii,”alisema Mheshimiwa Waziri.

Pia alisema, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi imeliona tatizo hilo, “hivyo kwa mamlaka niliyonayo ninazielekeza bodi zote za kitaaluma kuanzia Bodi ya Usajili wataalam wa mipangomiji, Baraza la Wapima Ardhi Tanzania na Bodi ya Usajili ya Wathamini kufanya uchunguzi wa kampuni zote zinazofanya kazi kinyume cha sheria ili hatua kali ziweze kuchukuliwa haraka.

“Aidha, naagiza makampuni binafsi ya upangaji,upimaji, makampuni mengine yanayojihusisha na masuala ya ardhi (Real Estate Agency) na mtu yeyoteanayejihusisha na uuzaji wa vipande vya ardhi kwa mtindo huo kusitisha kazi hizo haraka na kurejesha fedha za wananchi kwa maeneo ambayo wananchi wameingia kwenye kadhia hiyo.

“Kadhalika, nitoe rai kwa wananchi kuwa makini na watu wanaowauzia ardhi za namna hii. Naendelea kusisitiza kwamba kabla ya kununua ardhi yoyote hakikisha unapata taarifa na muongozo juu ya ardhi hiyo kutoka ofisi za ardhi zilizopo halmashauri au ofisi za ardhi za mikoa ili kupata ushauri,”alisema Waziri Dkt.Mabula.

Please follow and like us:
Pin Share