Na Mwandishi Wetu, Arumeru

Serikali imesikiliza kilio cha waliokuwa wafanyakazi katika shamba la Tanzania Plantation lilipo wilaya za Arusha na Arumeru mkoa wa Arusha kwa kuwapatia maeneo kwa ajili ya kujenga makazi, kilimo pamoja na ufugaji.

Akizungumza na wananchi wa kitongoji cha Lucy eneo la Bwawani wilayani Arumeru mkaoni Arusha tarehe 2 Agosti 2023 Dkt Mabula alisema, kutokana na uamunifu waliokuwa nao wananchi hao kwa muda mrefu katika eneo hilo kwa kuendelea kutunza mashamba hata pale wawekezaji walipotetereka serikali inakwenda kuwapatia maeneo ya kujenga nyumba zao za makazi na kumilikishwa kisheria.

Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa, kama hiyo haitoshi Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua kuwa wananchi hao bado ni wakulima na wana nguvu za kufanya shughuli za kilimo, ameelekeza pamoja na kupatiwa eneo la ujenzi wa nyumba wapatiwe pia walau ekari mbili kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Waziri Mabula alibainisha kuwa, katika eneo hilo la shamba la Tanzania Plantation Ltd wapo wananchi 486 waliovamia mashamba kwenye eneo hilo ambapo aliweka bayana kuwa, pamoja na ukiukwaji wa taratibu uliofanywa na wananchi hao Rais ameelekeza wazingatiwe katika kupatiwa maeneo kwa kufuata taratibu.

‘’Pia wapo wasamaria wema 27 waliojitolea maeneo yao kwa serikali ili kujengwa shule na zahanati ambapo nao imeelekezwa kuingizwa katika utaratibu wa kupatiwa maeneo’’. Alisema Dkt Mabula

Akifafanua zaidi, Dkt Mabula alisema kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi wa wananchi hao, serikali imeamua kuwapatia maeneo ya makazi kwa gharama ya shilingi 601 kwa mita moja ya mraba huku mashamba yakitolewa kwa shilingi milioni 2.5 kwa ekari moja.

By Jamhuri