Waziri wa Afya nchini Malawi alitoa taarifa kwa umma juu ya uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu tangu ulipothibitishwa mwezi Machi, 2022.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Aifello Sichalwe, imesema kuwa mlipuko umekwishaenea katika wilaya 25 nchini humo na jumla ya watu 4,604 wameugua na 132 kupoteza maisha kutokana na mlipuko huo.

Amesema kuwa kipindupindu ni ugonjwa hatari unaoambukizwa kwa kula chakula au kinywaji kilichochafuliwa na vimelea vya Vibrio Cholerae ambavyo husababisha ugonjwa huo. Vimelea hivi hupatikana kwenye kinyesi na matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu au mtu mwenye maambukizi ambaye bado hajaonesha dalili.

Amesema kuwa dalili kuu za ugonjwa wa kipindupindu ni kuharisha mfululizo kinyesi cha majimaji yanayofanana na rangi ya maji yaliyooshea mchele kisichotoa harufu, kutapika kwa mfululizo, homa, kulegea, kusikia kiu na kuishiwa nguvu. Mgonjwa anaweza kupoteza maisha endapo hatapata huduma ya matibabu ndani ya muda mfupi.

Amesema kuwa kutokana na mwingiliano wa shughuli za kiuchumi na kijamii uliopo baina ya watu wa Malawi na nchi ya Tanzania, Wizara ya Afya imetoa tahadhari dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu hususan katika mikoa na wilaya zinazopakana na nchi ya Malawi ili kuudhibiti usiingie na kuenea nchini.

“Kila mmoja anapaswa kuzingatia kuchemsha maji ya kunywa au kutibu kwa dawa maalumu na kuyatunza vizuri wakati wa matumizi.

“Kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji kwa kuoga, kufua kutupa taka, Kuepuka kula chakuka kilichopoa au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama,kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka na salama baada ya kutoka chooni.

Pia kuzingatia kunawa mikono kabla ya kutayarisha chakula cha watu wazima, wakati wa kumlisha mtoto, kuosha matunda kwa maji safi kabla ya kula, kuepuka utiririshaji wa maji kutoka chooni au kutupa taka ovyo au kuziacha taka kwa muda mrefu bila kuzipeleka dampo, tabia ambayo hupelekea mazalia ya inzi kuongezeka na kuhatarisha afya ya jamii kwani hueneza ugonjwa wa kipindupindu.

Wizara inawaagiza maafisa afya kusimamia usafiri wa mazingira katika maeneo yao pia inawakumbusha wananchi kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya juu ya kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali kwani kinga ni bora kuliko tiba.