Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Ikiwa ni siku ya mchangia damu Duniani Klabu ya Yanga imerudisha shukrani kwa jamii kwa kuchangia chupa 627 za damu na kuzitaka timu nyingine kuiga mfano huo kuokoa maisha ya watanzania.

Akizungumza leo June 14,2023 Jijini hapa katika maadhimisho ya siku ya mchangia damu duniani,Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema klabu ya Yanga imefanya jambo kubwa na la kiungwana kwa kuchangia chupa 627.

Waziri huyo amesema,”Injinia Hersi Saidi naomba nikupongeze wewe na Yanga kwa kuchangia chupa hizi za damu,mimi ni Simba lakini kama mngeshinda kule Algeria na kurudi na kombe ningehamia Yanga,”amesema.

“Mheshimiwa Nyongo (Stanslaus) Mwenyekiti wa Kamati ya Afya na Ukimwi tunapigwa hadi kwenye damu? tunatakiwa kujipanga msimu ujao,”alisema Waziri Ummy huku akicheka.

Klabu hiyo iliwakilishwa na Rais wake Inginia Hersi Said ambaye alipokea cheti na tuzo kwa kuchangia chupa hizo za damu.

Kwa upande wake Hersi aliwashukuru mashabiki wa klabu hiyo kwa kuchangia chupa hizo huku akidai klabu hiyo itaendelea kuchangia damu lengo likiwa ni kuokoa watanzania wenye changamoto ya damu.

“Na huu ni mwendelezo tu wa fadhira Kwa jamii yetu, tunatambua ni wajibu wetu kuokoa maisha ya wengine na hili tutalifanya kwa nguvu zote,na tunaomba mashabiki zetu wengine mtuunge mkono kuokoa maisha ya wengi zaidi,”amesema Rais huyo.

Siku ya Mchangia damu Duniani, hufanyika kila mwaka Tarehe 14/06 ya kila Mwaka ambapo kitaifa mwaka huu itafanyika hapa Dodoma, pamoja na shughuli zote za uhamashishaji na ukusanyaji damu,kumekuwa na zoezi la kuzindua Jengo la Kituo Cha Damu Salama Kanda ya Kati ambalo limeshaanza kutumika.

By Jamhuri