Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kilimanjaro

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Misitu na upandaji miti duniani ambayo kitaifa itafanyika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Same Machi 21, mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu akiwa wilayani Same kwenye ziara ya kukagua eneo litakalofanyika maadhimisho hayo pamoja na kukagua miradi ya maendeleo atakayotembelea Dkt. Mpango akiwa wilayani humo.

Aidha mkuu huyo wa mkoa amewataka wakazi wa Same na maeneo ya jirani kutumia vizuri nafasi ya kuwepo tukio kubwa la kitaifa la maadhimisho ya Siku ya Misitu na Upandaji Miti kushiriki kikamilifu ikiwemo kwa kupanda miti sehemu ya kuunga mkono kampeni za kitaifa za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni ameziomba kamati za maandalizi kufika kwa wakati eneo la tukio ili kushirikiana kwa pamoja na watendaji wengine wa Wilaya na Halmashauri sskuhakikisha maandalizi yanakamilika kwa wakati kama ilivyokusudiwa.

Maadhimisho hayo yataanza rasmi Machi 18 kwa kufanya shughuri mbali mbali ndani ya Wilaya ikiwemo utoaji wa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wananchi pamoja na miti inayopaswa kupanda kwenye maeneo yao kulingana na mazingira yake.

By Jamhuri