Siku za Kipande bandarini zahesabika

*Ni baada ya kuthibitika anatumia vibaya jina la Rais Kikwete, Ikulu

*Amuagiza Mwakyembe amchunguze, wafuatilia kumtukana Balozi

* Mtawa, Gurumo nao wakana, Mwakyembe adaiwa kumwogopa

*Aendelea kukaidi maagizo ya Bodi, amng’oa rasmi aliyeomba kazi yake

Na Deodatus Balile

Siku za Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Mzee Madeni Kipande (58), kuendelea kuwa madarakani zinazidi kuyoyoma baada ya Rais Jakaya Kikwete kukerwa na tabia yake ya kutumia jina la Rais kuhalalisha matendo yake yenye kukiuka sheria za utumishi wa umma.

Habari za uhakika kutoka Ikulu na kwa baadhi ya mawaziri waandamizi, zinasema Rais Kikwete baada ya kupata taarifa za Kipande kutumia vibaya jina lake, alichukia na kuamua kumwita Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, na kumpa maagizo mazito.

“Tena wala haikuwa siri, Rais alimwita Dk. Mwakyembe kama wiki mbili zilizopita mbele yetu mawaziri kama wanne hivi akamfokea,” kimesema chanzo chetu. “Alimpa maagizo ya wazi kuwa hafurahishwi na hataki jina lake litumiwe vibaya na Kipande kukandamizi watu wengine.

“Alimtaka Dk. Mwakyembe kufuatilia na kumpa taarifa juu ya utendaji wa kipande, na iwapo alidanganya kiwango cha mapato kuwa kimeongezeka, unyanyasaji wa wafanyakazi, kukaidi maagizo ya Bodi akidhani ana kinga ya Rais na kutamba kwenye corridor (viambaza) kuwa hakuna anayemueza yeye ana mizizi mizito.

“Baada ya maagizo hayo, Dk. Mwakyembe hakubisha, bali alimwambia Rais kuwa atatekeleza. Ninachokwambia hiki wala hakitiliwi shaka, hata Mwakyembe mwenyewe hawezi kujitokeza akasema hajaelekezwa, na iwapo hatatekeleza aliyoelekezwa na Rais basi ni wazi naye atakuwa anakaidi maelekezo halali ya Mheshimiwa Rais sawa na Kipande anavyokaidi maelekezo ya Bodi,” mmoja wa mawaziri waandamizi ameiambia JAMHURI, mwishoni mwa wiki.

Habari za uhakika kutoka Ikulu zinasema baada ya gazeti hili kuchapisha taarifa za unyanyasaji anaofanya Kipande bandarini na vifo vya wafanyakazi watatu —  Peter Gwamaka Kitangalala, Dotto Mbega  na mwingine aliyefahamika kwa jina la Oluwochi — kuwa wamefariki dunia katika kipindi cha miezi mitatu kutokana na shinikizo la damu lililozaa kiharusi baada ya vitisho vya Kipande, Rais Kikwete amesikitika mno na kusema hilo halipaswi kutokea.

“Rais alisema mtu anapofika mahala akasababisha kifo cha mtu, ama moja kwa moja au kwa njia yoyote, basi hiyo haivumiliki,” amesema mfanyakazi wa Ikulu, akisisitiza kuwa vyombo vya dola vinapaswa kuchunguza hali hiyo na ikibainika ni kweli hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya waliosababisha vifo hivyo.

“Baada ya Mtawa na Shaaban Gurumo kuona moto umewaka, wakaamua kuwaita wahariri wa gazeti linalomilikiwa na kuhaririwa na wazawa wa Bagamoyo, kwa nia ile ile ya kuendeleza ukabila kama mlivyoandika, akatumia gazeti linalohaririwa na mhariri anayetoka kijijini kwao kuthibitisha tuhuma dhidi yake bila kujua,” kimesema chanzo chetu.

Katika gazeti hilo la wiki, chapisho la Aprili 16 -22, 2014 Kipande hakukanusha tuhuma kuwa alimtukana Balozi wa Japan, Masaki Okada, au kuwa alimdanganya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe, kwamba mapato ya Bandari yamefikia Sh bilioni 50.

Wiki mbili zilizopita, Madeni Kipande amemtukana Balozi wa Japan nchini, Okada. Balozi Okada alikwenda ofisini kwa Kipande kumweleza nia ya Japan kutoa msaada wa kukarabati gati Na. 1-7 kama msaada, lakini kinyume cha matarajio kwamba Kipande angepokea msaada huo, aliishia kumrushia matusi Balozi wa Japan.

“Kwanza alikuwa amekataa kumuona huyo Balozi, akisema aonane na wasaidizi wake, lakini Balozi aliposisitiza msaidizi wa Kipande akamwambia protokali zinamtaka amuone, akakubali kumuona. Kilichotokea baada ya hapo kilikuwa kituko. Balozi alimweleza kuwa anataka nchi yake isaidie kukarabati gati Na. 1-7 la bandari. Kipande akamwambia Bandari ilitangaza zabuni, na Japan kama ilikuwa inataka kufanya hivyo ilipaswa kuomba zabuni na kuingia kwenye ushindani.

“Balozi alisisitiza kuwa nia yake ni kutoa msaada si kufanya biashara, Kipande akasema huo ni uongo kwani amezoea kauli za aina hiyo na ni ujanja wa kupenyeza rushwa na kuzipatia kazi kampuni za Kijapani kwa njia za panya, hivyo yeye hatakubali kama Japan inataka kutoa msaada wa ukarabati wa bandari basi isubiri zabuni ijayo.

“Kauli kwamba Japan inataka kutumia mkondo wa ubalozi kwa njia ya rushwa kuzipatia kampuni za nchini kwake kazi wakati nchi hiyo ililenga kutoa msaada ilimuuma mno Balozi, na taarifa zilizopo anataka au tayari ameandika barua kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kutaka ufafanuzi kwanini nchi yake ya Japan ihusishwe na rushwa kwa kutaka kuisaidia Tanzania,” kimesema chanzo chetu.

Afisa Mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ameiambia JAMHURI kuwa wizara yake inalishughulikia kwa nguvu suala hilo kunusuru uhusiano wa Tanzania na Japan.

“Tanzania na Japan zimekuwa nchi marafiki na taifa hili limekuwa msaada mkubwa kwetu. Leo kumtukana Balozi na nchi yao ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu. Tunalishughulikia hili na Kipande ni lazima ataondolewa angalau kwa kosa hili linaloweza kuigharimu Tanzania katika dunia ya diplomasia tusipochukua hatua,” amesema afisa huyo.

Kuhusiana na kifo cha Mbega, gazeti hilo likimnukuu mtu waliyemwita mtaalamu au daktari wa binadamu, lilikiri uwezekano wa kifo cha Mbega kutokana na shikizo la Kipande, liliposema: “Kwa hili [la kifo cha Mbega] naweza kukubaliana na wewe kitaalamu, maana huyu alikuwa ni mtu wa karibu na hazina ya Bandari na sasa fedha zimeibwa kwa mamilioni, wewe ndiye uliyekuwa mlinzi wa lango la fedha sasa zimepotea, iwe umeiba wewe au umeibiwa na hasa kama umeibiwa ni lazima uchanganyikiwe na hata kupata shinikizo la damu linaloweza kukusababishia kifo,” mtaalamu alifafanua kupitia gazeti hilo.

Kipande aikaidi Bodi

Desemba 2012, Kipande alimsimamisha kazi mtumishi wa Idara ya ICT, Marcelina Mhando. Baada ya uchunguzi, Bodi ya Wakurugenzi ilibaini kuwa taratibu za kuingia kwenye ajira kwa Mhando zilikuwa na tatizo ila hakuwa na tatizo lolote la kinidhamu, hivyo Bodi ya Wakurugenzi Mei 15, 2013 ikaagiza Mama Mhando arejeshwe kazini ila apunguzwe cheo ngazi moja.

Cha kusikitisha, Kipande ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu na hivyo kuwa Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi, alisikika akisema kuwa kamwe hatamrejesha kazini mtumishi huyo.

“Kimsingi kama kuna kitu kimenishangaza ni hiki. Sisi Bodi ya Wakurugenzi tunapaswa kusimamia biashara na masuala ya Bandari, hivyo Mkurugenzi Mkuu anaripoti kwenye Bodi na anapaswa kutekeleza maagizo ya Bodi, lakini hadi leo ni karibu mwaka sasa amegoma kumrejesha kazini huyu Mama Mhando.

“Anaendelea kumlipa mshahara na stahiki zake zote, hafanyi kazi huyu mama si kwa yeye kukataa bali kutokana na Kipande kukaidi maagizo ya Bodi. Sasa najiuliza, Bodi ina maana gani ya kuwapo? Waziri Mwakyembe analifahamu suala hili, lakini naye taarifa nilizonazo anamuogopa Kipande kwani anamtisha kuwa yuko karibu na Rais,” mjumbe wa Bodi ameiambia JAMHURI.

JAMHURI ilipowasiliana na baadhi ya wajumbe wa Bodi, ilielezwa kuwa wengi wamekata tamaa kuitumikia Bodi hiyo, na wanakuwa na wasiwasi kuwa huenda kwa kuwa Kipande alisoma darasa moja na Profesa Joseph Msambichaka, kwa sasa lao ni moja, hivyo wameamua kuweka pamba masikioni.

Kwa upande wake, Profesa Msambichaka ambaye kikazi yuko Mbeya, akipigiwa simu hapokei au anapokea na kuiacha hewani bila kuzungumza. Mwandishi wa habari hizi amempelekea barua pepe Profesa Msambichaka kuomba ufafanuzi juu ya tuhuma hizi na sasa imepita miezi miwili hajajibu barua pepe zote mbili.

Katika kinachoelezwa kuwa Kipande ana chuki na wanawake na ana nguvu kuliko Waziri Mwakyembe, mwaka jana alishinikiza Bodi ya Wakurugenzi ikavunjwa na kuondoa wakurugenzi asiowataka, kisha akamshinikiza Dk. Mwakyembe kuteua wajumbe anaowataka yeye.

Baada ya kujihakikishia kuwa wanawake wameondolewa kwenye Bodi, alimshinikiza Waziri Dk. Mwakyembe akateua wanaume tu, walioungana na Profesa Msambichaka ambaye ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya.

Pamoja na Profesa Msambichaka, wengine kwenye Bodi ya sasa inayomwogopa Kipande isiyo na meno, iliyotoa maagizo akayakaidi na ikaendelea kuwapo kwa kuwa wanapata posho, ni Said Sauko, ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa TAZARA na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia.

Pia wamo Jaffer Machano, ambaye ni Meneja wa TIB, Mhandisi Amani Kisamfu, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa TRL na Edmund Njowoka, ambaye ni mfanyakazi wa kawaida wa TPA, ila ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Bandarini Tanzania (DOWUTA).

Dk. Mwakyembe kumuogopa Kipande

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa Dk. Mwakyembe anamuogopa Kipande kutokana na historia yake katika mchakato wa mwaka 2005, ambapo anaona kupewa uwaziri ni sawa na hisani kwake, hivyo anaona pengine akimkorofisha Kipande anaweza kumchongea kwa Rais Kikwete akamuondoa madarakani.

“Unajua Mwakyembe alikuwa Mwenyekiti wa kampeni za Profesa Mwandosya mwaka 2005. Alifanya kila mbinu za kumhujumu Rais Jakaya Kikwete, ila akashindwa. Leo, anaona Rais Kikwete amempa hisani ya kumteua kuwa waziri, anaona akikorofisha ndugu wa Rais Kikwete anaweza akanyang’anywa tonge, hivyo anaona bora afunike kombe mwanaharamu apite,” kimesema chanzo chetu.

JAMHURI ilipowasiliana na Dk. Mwakyembe kuhusiana na tuhuma hizi na nyingine, kwanza alikataa kutoa miadi, kisha akawa hapokei hata simu na alipotumiwa ujumbe wa maandishi, alijibu kwa ufupi hivi: “Ulishamhukumu [Kipande] tayari bila kutuuliza. Endelea tu.”

Kwa upande wake, Kipande alipoulizwa na JAMHURI, alisema maswali anayoulizwa ni ya kitoto na akawa kila akitoa miadi anaikiuka kudhihirisha kiwango cha kiburi.

Kama inavyosema taarifa ya mmoja wa waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi iliyochapishwa kwenye gazeti hili, tangu mwaka 2008 hadi leo kamera za CCTV hazifanyi kazi bandarini na hii imethibitishwa na Mkurugenzi wa ICT, Phares Magesa, kuwa ni kweli.

Mita za kupimia mafuta yanayoingizwa nchini nazo hazitumiki kwa zaidi ya miaka mitatu sasa na mifumo ya kuingiza na kutoa mizigo bandarini haiwasiliani, huku Kipande na Magesa wakiendelea kupuuza maagizo ya Bodi ya Wakurugenzi waliotaka atafutwe mshauri wa kukagua mfumo wa ICT na kutoa mapendekezo.

Hadi sasa maagizo ya Kamati ya Mbakileki iliyoundwa na Waziri Mwakyembe kuchunguza utendaji wa Bandari ambayo mapendekezo yake yalimfanya Waziri kuvunja Bodi iliyokuwapo na kufukuza viongozi wakuu wa Bandari, hadi leo haijatekelezwa hata kwa asilimia 10. Hali bandarini inazidi kuwa mbaya.

Kipande amsimamisha aliyeomba kazi yake

Kipande kwa upande mwingine, wiki iliyopita alikuwa na furaha ya aina yake baada ya kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Masoko, mama Francisca Muindi. “Kwenye mkutano wa watendaji wakuu juzi alitamba kweli. Akasema amemng’oa mama Muindi na alitumia maneno kuwa ameng’oa kisiki na mizizi yake. Akatamba kuwa kuanzia sasa yeyote asiyekubaliana naye atang’olewa tu.

“Mameneja na wakurugenzi wote walikaa kimya wakasikiliza tambo zake, isipokuwa Mkurugenzi swahiba wake yeye alisema; ‘Kweli bosi mtu asiye pamoja na sisi ni lazima tumuondoe.’ Hili lilitushangaza wengi. Tunajua anamfukuza mama Muindi si kwa sababu hana uwezo, bali kwa sababu aliomba kazi ya Ukurugenzi Mkuu ilipotangazwa.

“Hata [Hassan] Kyomile aliyeomba nafasi hiyo, naye alishushwa cheo kutoka Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi na kupelekwa kuwa Meneja wa Bandari ya Tanga. Hii imetusikitisha wengi, tunajiuliza ni kosa lipi walilolifanya? Bodi ya Wakurugenzi ilikwishakemea hili, lakini naona labda lina kinga ya Waziri.

“Tulipata taarifa kuwa Waziri Mwakyembe alikuwa anataka kufinyanga utaratibu kumfurahisha Bwana Mkubwa [Rais Kikwete] kwa kuwaondoa wote walioomba kazi hii kisha Kipande apewe kuwa hakuwa na mshindani, lakini walipofikia kwenye eneo la sifa na vyeti walivyonavyo, ikabainika Kipande ni msindikizaji.

“Kipande aliwasilisha hata certificate of attendance (vyeti vya mahudhurio) vya saa mbili alivyopewa kwa kuhudhuria semina, akakuta wenzake wanawasilisha vyeti vya uhakika, hivyo kigezo hiki wakashindwa kukitumia kuwaondoa. Mchakato wenyewe ni kama umekufa, maana tunasikia Kipande anazo tuhuma nyingi kwenye ofisi alikotokea, hivyo bado vyombo vya dola vinamchunguza,” amesema mmoja wa maafisa waandamizi, aliyekuwa kwenye kikao cha wiki iliyopita wakati Kipande anatamba.

Hadi sasa, inaelezwa kuwa Kipande hajaibuka na mkakati mpya wa kuifanya Bandari kuwa na mapato mapya, zaidi ya kuacha wateja waje wenyewe na wengi hawavutiwi na Bandari ya Dar es Salaam kutokana usalama wa mizigo yao kuwa hatarini.

Hata mizigo ya Tanzania, mingi imeanza kupitia Mombasa. Kiwango cha mizigo ya Tanzania inayopitishiwa Mombasa kimeongezeka hadi asilimia mbili ya mzigo wote kwa mwaka.

Je, unajua kwanini Mwakyembe alimwandikia barua ya onyo Kipande? Usikose toleo la wiki ijayo ushuhudie Mkurugenzi huyu anavyoendesha Bandari kama familia isiyo na mwelekeo.