Hotuba ya Lissu iliyosababisha TBC1 ‘izimwe’

Aprili 12, mwaka huu, Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Tundu Lissu aliwasilisha maoni ya Wajumbe walio wachache katika Kamati Namba Nne kuhusu sura ya kwanza nay a sura ya sita ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati akiwasilisha, Televisheni ya Taifa (TBC1) ilikata matangazo yake katika kile kilichotafsiriwa na wengi kuwa ni kuuepusha umma kupata maoni ‘makali’ yaliyomo kwenye hotuba ya Lissu. Kwa kuzingatia haki ya wananchi ya kupata habari, JAMHURI inawaletea hotuba hiyo neno kwa neno. Endelea

UTANGULIZI

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (‘Rasimu’) ndizo msingi ambao Rasimu yote imejengwa juu yao. Wakati Sura ya Kwanza inagusa suala la muundo wa Muungano katika ibara moja tu kati ya ibara tisa, Sura yote ya Sita inahusu ‘Muundo wa Jamhuri ya Muungano.’ Suala la Muungano na hasa Muundo wake limetawala mjadala wa kisiasa na kikatiba wa Tanzania kwa zaidi ya miaka thelathini. Ndio maana katika waraka wake wa siri kwa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (‘CCM’), Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya chama hicho imetamka kwamba “muundo wa Muungano ndiyo moyo wa Rasimu na ndiyo unaoamua ibara nyingine zikae vipi.”

Suala hili pia limetawala mchakato wa Katiba Mpya tangu ulipoanza miaka mitatu iliyopita. Kama alivyosema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Joseph Sinde Warioba wakati wa kuwasilisha Ripoti ya Tume yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar tarehe 30 Disemba, 2013: “Moja ya mambo ambayo yamejadiliwa sana na kwa hisia kali tangu Rasimu ya awali ilipotolewa … ni Muungano wa Tanzania. Jambo kubwa limekuwa juu ya muundo wa Muungano.”

Umuhimu wa suala hili unathibitishwa pia na uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalum kuelekeza kwamba Kamati zake Namba Moja hadi Kumi na Mbili zianze kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu. Haya ni maoni ya wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne juu ya Sura hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Mjadala wa Kamati Namba Nne kuhusu Sura za Kwanza na Sita za Rasimu unathibitisha pia umuhimu wa suala la muundo wa Muungano katika mjadala mzima wa Rasimu. Kama Taarifa ya Kamati yetu inavyoonyesha, Kamati Namba Nne imeshindwa kufanya uamuzi kuhusu suala hili katika ibara za 1 na 60 za Rasimu. Katika ibara ya 1 ya Sura ya Kwanza, wajumbe walio wengi walipata kura 22, ambayo ndiyo theluthi mbili ya kura za wajumbe wote 33 wa Tanzania Bara wa Kamati Namba Nne. Kwa upande wa Zanzibar, wajumbe walio wengi walipata kura 9 ambayo ni pungufu ya kura 13 zinazohitajika ili kufikisha idadi ya theluthi mbili ya wajumbe wote 19 wa Zanzibar.

Kwa upande wa ibara ya 60, wajumbe walio wengi walipata kura 22 za wajumbe kutoka Tanzania Bara, ambazo ni theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote 33 kutoka Tanzania Bara. Aidha, kwa Zanzibar, wajumbe walio wengi walipata kura 8, ambazo pia ni pungufu ya kura 13 zinazotakiwa kufikisha idadi ya theluthi mbili ya wajumbe wote 19 kutoka Zanzibar. Kwa sababu hiyo, ibara za 1 na 60 za Rasimu hazikupitishwa au kuamuliwa na Kamati Namba Nne kama inavyotakiwa na kifungu cha 26(2) cha Sheria na kanuni ya 64(1) ya Kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Sasa tunaomba kwa ridhaa yako, tuwasilishe hoja na sababu za maoni ya wajumbe walio wachache katika Kamati Namba Nne kuhusu Sura hizi mbili ambazo ndio ‘moyo wa Rasimu.’

SURA YA KWANZA

Sura ya Kwanza ya Rasimu inahusu ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Sehemu ya Kwanza ya Sura hiyo inazungumzia ‘jina, mipaka, alama, lugha na tunu za Taifa.’ Ibara ya 1 inaitambulisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ibara ya 2 inatangaza ‘eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’; na ibara ya 3 inaweka utaratibu wa ‘alama na sikukuu za Taifa.’ Vile vile ibara ya 4 inaweka utaratibu wa lugha ya Taifa na lugha za alama, wakati ibara ya 5 inahusu ‘tunu za Taifa.’

Kwa upande wake, Sehemu ya Pili ya Sura ya Kwanza inaweka masharti ya ‘mamlaka ya wananchi, utii na hifadhi ya Katiba. Ibara ya 6 ya Sehemu hiyo inatoa ufafanuzi wa ‘mamlaka ya wananchi’; ibara ya 7 inafafanua uhusiano kati ya ‘watu na Serikali’; ibara ya 8 inashurutisha ‘ukuu na utii wa Katiba’; na ibara ya 9 na ya mwisho inaweka ‘hifadhi ya utawala wa Katiba.’

IBARA YA 1

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kama maelezo yake ya pembeni (marginal note) yanavyoonyesha, ibara ya 1 inaitambulisha ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Ibara ya 1(1) inatamka kwamba “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho lenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati za Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.”

Kwa upande wake, ibara ya 1(2) inafafanua kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania “ni Shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na lisilofungamana na dini.” Mwisho, ibara ya 1(3) inatukumbusha kwamba “Hati ya Makubaliano ya Muungano … ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba hii, kwa kadri itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa Makubaliano hayo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne wanapendekeza mabadiliko ya jina la nchi yetu kutoka jina la sasa la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ kuwa jina jipya la ‘Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.’ Aidha, wajumbe hao wanapendekeza kuacha kutajwa kwa Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 katika ibara ya 1(1) na (3) ya Rasimu. Badala yake, inapendekezwa kwamba Katiba hii ndiyo iwe msingi wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.

Kwa mapendekezo haya, ibara ya 1(1) itasomeka kama ifuatavyo: “Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni Shirikisho ambalo limetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.” Kwa mantiki hiyo, ibara ya 1(2) itasomeka: “Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni Shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na lisilofungamana na dini.” Aidha, ibara ya 1(3) itasomeka: “Katiba hii ndio msingi mkuu wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.” Zifuatazo ni hoja na sababu za mapendekezo haya.

SHIRIKISHO AU MUUNGANO?

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Katika nusu karne ya uhai wake, nchi yetu imeitwa ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Hata hivyo, katika kipindi chote hicho, Katiba na Sheria za nchi yetu hazijawahi kufafanua kwa uwazi aina au haiba ya ‘Muungano’ huu. Matokeo ya kukosekana kwa ufafanuzi huu ni kwamba katika nusu karne hiyo, kumekuwa na mjadala mkubwa wa kikatiba, kisiasa na kitaaluma kuhusu suala la kama Jamhuri ya Muungano ni dola ya muungano (a unitary state), au ni dola ya shirikisho (a federal state). Majibu ya swali hili yamekuwa na athari za moja kwa utambulisho, haki, maslahi na wajibu wa Washirika wa Muungano huo, yaani Tanganyika na Zanzibar, na hasa kwa wananchi wa nchi hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kukosekana kwa ufafanuzi wa aina ya muungano wetu haujawa suala la mijadala ya kisiasa na kikatiba peke yake, bali kumekuwa ni chanzo cha migogoro mikubwa ya kisiasa baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Migogoro hii ilianza tangu mwanzo kabisa wa Muungano wakati wa sakata la kuwa na ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi kwa upande wa Tanganyika na ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki kwa upande wa Zanzibar.

Aidha, kati ya mwaka 1964-1967 ulizuka mgogoro mkubwa kuhusiana na uwakilishi wa Zanzibar katika iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na uanzishwaji wa Benki Kuu ya Tanzania; kuunganishwa kwa vyama vya ASP na TANU na kuundwa kwa CCM mwaka 1977, na katika mjadala wa marekebisho ya Katiba wa mwaka na baadae ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ mwaka 1983/1984.

Baadae mwaka 1988 ulitokea mgogoro mkubwa uliopelekea kung’olewa madarakani kwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad na baadae kufukuzwa katika CCM; wakati wa harakati za kudai kura ya maoni kuhusiana na Muungano mwaka 1989/1990; wakati wa mjadala wa kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1991; wakati wa sakata la Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (Organization of Islamic Countries – OIC) mwaka 1993; wakati wa mjadala wa G-55 na madai ya kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano mwaka 1994, na Uchaguzi Mkuu wa 1995 huko Zanzibar.

Milenia Mpya ilipoanza ilianza na mgogoro kuhusu matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 uliopelekea mauaji ya Januari 2001 huko Zanzibar. Mgogoro huo ulifuatiwa na mgogoro juu ya suala la ugunduzi wa mafuta visiwani Zanzibar; harakati za kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki na hivi karibuni kupitishwa kwa Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 mwaka 2010.

Zaidi ya migogoro hii, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Mapinduzi zanzibar zimeunda tume na kamati nyingi ili kupata dawa ya ‘Kero za Muungano.’ Serikali ya Mapinduzi Zanzibar peke yake imeunda tume na kamati 13 katika kipindi kifupi cha miaka 12 kuanzia mwaka 1992 hadi 2004; wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeunda tume na kamati nane kushughulikia matatizo hayo. Licha ya jitihada zote hizo, ‘Kero za Muungano’ hazijapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Tangu miaka ya mwanzo ya Jamhuri ya Muungano kulikuwa na mitazamo miwili tofauti miongoni mwa waasisi na viongozi wakuu wa Jamhuri ya Muungano. Mitazamo hii tofauti inathibitishwa na kauli ya Mwalimu Julius K. Nyerere, mwasisi na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano katika Mkutano Maalum wa Halmashauri Kuu ya CCM uliofanyika Dodoma kati ya tarehe 24-30 Januari, 1984: “… Muungano wa Tanzania ukiangalia kwa jicho la Zanzibar ni wa shirikisho lakini ukiangalia kutoka upande wa Tanzania Bara ni Serikali moja.”

Mwalimu alikuwa akimjibu Makamu Mwenyekiti wa CCM, Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar wakati huo, Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi aliyesema kwamba Muungano wa Tanzania umeunda Shirikisho (Federation) na sio Serikali moja (Unitary State). Mjadala huo ulipelekea ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ na kung’olewa madarakani kwa Jumbe, Waziri Kiongozi wake Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu Bashir Kwaw Swanzy. Aidha, Wolfgang Dourado, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati Hati ya Muungano inasainiwa, na mkosoaji mkubwa wa Muungano huo, aliwekwa kizuizini kwa kuunga mkono hoja za Rais Aboud Jumbe.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Miaka kumi baada ya ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ Jamhuri ya Muungano ilikabiliwa na mgogoro mwingine tena wa kikatiba na kisiasa, mara hii ukitokana na Zanzibar kujiunga na OIC. Kitendo hicho kilizua tafrani kubwa ya kisiasa pale Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipopitisha Azimio la kutaka kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano mwezi Agosti, 1993. Azimio hilo liliungwa mkono na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kitendo kilichomfanya Mwalimu Nyerere kuingilia kati na kuzima jaribio hilo.

Baadaye Mwalimu aliandika kitabu alichokiita Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania kilichochapishwa mwaka 1994. Katika kitabu chake, Mwalimu anarejea mkanganyiko ambao umekuwepo kuhusu aina ya Muungano huu kwa maneno yafuatayo:

“Nchi zinapoungana na kuwa nchi moja mifumo ya kawaida ya miundo ya Katiba ni miwili: Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake, na nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja. Katika mfumo wa pili kila nchi itajivua madaraka fulani ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho, na itakuwa na serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki. Mambo yatakayoshikwa na serikali ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka ya nchi zilizoungana, basi kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi moja, bali zinaendelea kuwa nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani…. Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni nchi moja yenye serikali tatu, Serikali ya shirikisho na serikali mbili za zile nchi mbili za awali zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Mwaka ambao Mwalimu Nyerere alichapisha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, Makamu Mwenyekiti wake wa CCM na Makamu Rais wake hadi Januari 1984, Alhaj Aboud Jumbe, aliyekuwa pia Waziri wa Afya wa Zanzibar wakati Muungano unazaliwa na baadae Rais wa Pili wa Zanzibar, naye alichapisha The Partnership: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Miaka 30 ya Dhoruba. Katika kitabu hicho, Alhaj Jumbe anathibitisha kwamba “Ibara za Mkataba wa Muungano ziliweka bayana mfumo ambao serikali kuu na serikali shiriki katika Muungano kuwa na nguvu zinazoendeana, yaani, mfumo wa shirikisho ambao kuna mgawiko wa mahakama, baraza la kutunga sheria na urais baina ya serikali kuu na serikali mbili au zaidi, na kila serikali ikiwa na nguvu kamili ndani ya mamlaka yake.”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Aina ya dola iliyotokana na Hati ya Makubaliano ya Muungano haikuwahangaisha waasisi wa Muungano ama viongozi wake wakuu peke yao. Hata ndani ya makorido ya mamlaka, mjadala juu ya suala hili umekuwa mkubwa na umeundiwa Tume na Kamati mbali mbali za kulichunguza. Kwa mfano, hata kabla ya kuchapishwa kwa Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania na The Partner-ship, tarehe 6 Aprili, 1992, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Salmin Amour aliunda Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Kujenga Hoja Juu ya Masuala ya Muungano wa Tanzania, maarufu kama Kamati ya Amina Salum Ali kutokana na jina la Mwenyekiti wake. Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna, ambaye ni mjumbe wa Bunge hili Maalum, alikuwa Katibu wa Kamati hiyo.

Pamoja na mambo mengine, Kamati ya Amina Salum Ali ililichunguza suala la aina ya Muungano uliozaliwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano. Jibu la Kamati hiyo lilikubaliana na nusu ya hoja ya Mwalimu Nyerere na nusu ya hoja ya Alhaj Aboud Jumbe: “… Muungano wa Tanzania, haidhuru unaitwa ‘Union’, lakini uko kati na kati baina ya ‘Union’ na Shirikisho. Kuwepo kwa Serikali ya Muungano yenye madaraka makubwa ni kielelezo cha sura ya ‘Union’. Sura hii inazidi kutiliwa nguvu na kile kitendo cha Tanganyika kuvua madaraka yake yote na kuyaingiza katika Serikali ya Muungano. Kwa upande mwengine kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye madaraka kamili Zanzibar juu ya mambo yote yasiyokuwa ya Muungano, ni kielelezo dhahiri cha sura ya Shirikisho. Kwa hivyo, Muungano huu ni wa aina yake.”