Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Singida

Shirika lisilo la kiserikali la HELVETAS – Tanzania limegawa bure miche 1,700 ya miti ya matunda kwa wakulima wa wilaya tatu za Mkoa wa Singida kama utekelezaji wa mradi wa mazingira wa UKIJANI unaolenga kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Pamoja na kutoa miche ya miti ya matunda, shirika hilo pia limegawa vifaa mbalimbali kwa wakulima hao vinavyotumika katika shughuli za kilimo cha bustani kama matoroli, mapipa ya maji, mikasi na majagi ya kumwagilia maji (water canon).

Sehemu ya miche hiyo ya miti ya matunda na vifaa vya kilimo cha bustani ilikabidhiwa kwa wakulima mwishoni mwa wiki katika Kijiji cha Puma, Wilaya ya Ikungi na ofisa mradi huo wa Shirika la HELVETAS – Tanzania, Maximillian Saku, katika tukio ambalo pia lilishuhudiwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Stanislaus Choaji.

Miche ya miti ya matunda iliyogawiwa na kusambazwa ni pamoja na mipapai 1,000, miembe 300, malimao 200 na michungwa 200.

Akizungumza katika tuko hilo la makabidhiano, ofisa miradi huyo alisema moja ya malengo ya mradi huo wa UKIJANI ni kuwawezesha wanawake kuongeza fursa za kiuchumi, maarifa na ushirikishwaji zaidi, ikiwa ni pamoja na uongozi katika kufanya uamuzi wa jamii.

“Mradi wa UKIJANI pia umelenga kuboresha matumizi bora ya ardhi katika vijiji, hasa kulinda mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuchangia kuboresha maisha ya familia na kurejesha mazingira yaliyoharibika katika wilaya za Manyoni, Ikungi na Iramba katika Mkoa wa Singida,” amesema mratibu huyo.

Ameongeza: “Pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali kuhusu sera na utunzaji wa mazingira, mradi huu pia umelenga kuwawezesha na kuwajengea uwezo wanawake kupata hatimiliki za ardhi ili wafanye shughuli za ujasiriamali kwa weledi na kujiamini zaidi.”

Amesema mradi unatarajiwa kuwanufaisha wananchi wa wilaya hizo, kuongeza ufahamu na kujenga uwezo juu ya umiliki wa ardhi, maliasili na haki za usimamizi wa rasilimali, pamoja na kuwezesha ushiriki wa sauti ya wanawake katika michakato ya uamuzi katika masuala ya kijamii.

Ameongeza kuwa pia wanatarajia mradi huo utawasaidia wanawake kujihusisha na kilimo endelevu cha bustani na misitu na wanawake kupata huduma mbalimbali za kijamii kwa urahisi kama huduma za ugani, pembejeo, uzalishaji wa biashara, fedha na mazingira.

Kwa upande wake, Choaji, aliwataka wakulima waliobahatika kupata fursa hiyo kufanya mradi huo kuwa endelevu ili uweze kuleta manufaa katika jamiii wanayoishi.

“Wito wangu kwenu ni kwamba mtumie mradi huu vizuri na kuwa endelevu ili ulete mabadiliko chanya kijamii na kiuchumi, kwa kuwa tuna historia ya miradi ya aina hii kufa pamoja na wafadhili kuchangia fedha zao,” amesema Choaji.

Kwa upande wa mmoja wa wakulima hao, Rustica Samwel, kutoka Kijiji cha Muhintiri, Wilaya ya Ikungi, amesema kupitia mradi huo wanatarajia kubadilisha maisha yao kutokana na fursa kubwa iliyoko katika kilimo cha bustani na misitu.

Mradi huo ambao unafadhiliwa, unatarajiwa kufikia mwisho mwaka 2026, na unatarajiwa kuwafikia walengwa 5,000 ambapo wanawake ni 3,000 na vijana zaidi ya 2,000 wenye umri kati ya miaka 18 – 35.

By Jamhuri