Watanzania jitokezeni kutoa maoni miswada ya sheria ya uchaguzi na vyama vya siasa – Dk Biteko

πŸ“Œ Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia

πŸ“Œ Ataka Wananchi kuchagua viongozi bora katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbogwe, Geita

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa Watanzania kushiriki katika kutoa maoni kuhusu muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2023 ili kuunga mkono jitihada za Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kujenga Tanzania iliyo bora zaidi katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Dkt. Biteko amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita katika Sherehe za kuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka 2024 zilizoandaliwa na Mbunge wa Mbogwe, Mhe. Nicodemus Maganga ambazo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali mkoani Geita wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Martine Shigella.

β€œMhe. Rais amepeleka miswada hii bungeni iliyosomwa wakati wa Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge na tangazo limeshatoka la kuwaomba wananchi kwenda kutoa maoni yao bungeni kuanzia tarehe 6 hadi 10 Januari 2024 kuhusu marekebisho ya sheria hizi, niwaombe watanzania, nendeni mkatoe maoni yenu ili kujenga Tanzania iliyo bora kuliko kubaki nyuma kulalamika.” Amesisitiza Dkt. Biteko

Amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzania wa vyama, dini na makabila mbalimbali, vilevile anasikiliza malalamiko ya makundi mbalimbali na kuyafanyia kazi akitolea mfano suala la kuruhusu Vyama vyote vya Siasa nchini kufanya mikutano ya hadhara ili kueleza sera zao na kwamba nia ya Rais ni kujenga mshikamano na umoja nchini.

Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu, Dkt. Biteko ametoa wito kwa wananchi kuchagua viongozi walio bora na kwamba watu wasigawanyike na kufarakana sababu ya uchaguzi, bali waungane katika uchaguzi huo kwa kuzungumza yale yanayowaunganisha kama vile barabara, maji, umeme na wasiruhusu mtu kupandikiza chuki katikati yao.

Katika salam zake za mwaka 2024, Dkt. Biteko ameendelea kusisitiza kuhusu watanzania kupendana, kuthaminiana, kuvumiliana, kusameheana, kuwa na shukrani, kusaidiana na kumfanya mtu mwingine afurahi, huku lengo likiwa ni kujiletea maendeleo kwa pamoja.

Kuhusu hali ya upatikanaji umeme wilayani Mbogwe, Dkt. Biteko amesema kuwa, itaendelea kuimarika kwani imejengwa njia mpya ya umeme ambayo itapeleka umeme wilayani humo kutokea kituo cha Nyakanazi, pia itajengwa njia nyingine ambayo itapeleka umeme Mbogwe kutokea Kahama na pia kitajengwa kituo cha kupoza na kusambaza umeme wilayani humo kama ambavyo ujenzi wa vituo hivyo utakavyofanyika katika wilaya nyingine nchini.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella akiwasilisha salam za Mwaka Mpya 2024 alisema anaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye wilaya ya Mbogwe ikiwemo miradi ya Elimu, Maji, Umeme, Barabara pamoja na Afya.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani Geita, Shigella amesema kuwa, asilimia 90 ya vijiji vya mkoa wa huo tayari vimeshapatiwa umeme na vijiji 50 vilivyosalia kazi za kusambaza umeme zinaendelea ikijumuisha mipango ya kupeleka umeme hadi kwenye vitongoji.

“Tunamshukuru Rais, Dkt. Samia amefanya kazi kubwa kuleta fedha za maendeleo mkoani Geita na tunaahidi kuendelea kusimamia miradi yote ili itekelezwa kwa wakati. ” Amesisitiza Shigella

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbogwe, Mhe. Nicodemus Maganga, amemshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kufika Mbogwe kushiriki na wananchi katika sherehe hizo na kuongeza kuwa wilaya ya Mbogwe imejipanga vizuri katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo Sekta ya Madini kuendelea kufanya vizuri.

Amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya nchini na kwa kupeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo wilayani Mbogwe huku akiongeza kuwa, wanajipanga kuifanya wilaya ya Mbogwe kuwa yenye mabadiliko makubwa ifikapo mwaka 2027.