Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mkoa wa Singida umeweka historia ya maendeleo kwa kutumia zaidi ya shilingi trilioni 1.72 katika kipindi cha miaka mitano (2020/21 hadi 2024/25), fedha zilizotolewa na Serikali Kuu, mapato ya ndani pamoja na michango kutoka kwa wadau wa maendeleo kwa ajili ya uendeshaji na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

Hayo yameelezwa leo Julai 4,2025 jijini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya serikali ya awamu ya Sita kwenye mkoa huo ambapo kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi trilioni 1.055 kilitolewa na Serikali Kuu moja kwa moja, huku wastani wa utekelezaji wa bajeti ukiwa ni asilimia 95 katika kipindi hicho cha miaka mitano.

Dendego ameeleza kuwa ongezeko la fedha hizo limeleta mapinduzi makubwa katika sekta za kilimo, uchumi, huduma za jamii, miundombinu na utawala bora, kwa lengo la kuimarisha ustawi wa wananchi na kuongeza fursa za ajira na kipato.

Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2020/21, Serikali ilitoa shilingi bilioni 153.8 kati ya bilioni 180.2 zilizotengwa (85%), wakati mwaka 2021/22 uliona utekelezaji wa asilimia 102 baada ya Serikali kutoa shilingi bilioni 202.4 dhidi ya bajeti ya bilioni 199.4.

“Mwaka 2022/23, shilingi bilioni 221.6 zilitolewa, sawa na asilimia 92 ya bajeti, huku mwaka 2023/24 ukiongoza kwa utekelezaji wa asilimia 105, ambapo shilingi bilioni 241.6 zilitolewa. Kwa mwaka wa mwisho wa kipindi hicho, 2024/25, mkoa ulipokea shilingi bilioni 236.3 kati ya bilioni 259.3 zilizopangwa, sawa na asilimia 91 ya bajeti, “ameeleza

Ameeleza kuwa Matokeo ya uwekezaji huo yameonekana kwenye ukuaji wa uchumi wa mkoa ambapo pato la ndani (Regional GDP) limeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.709 mwaka 2020/21 hadi shilingi trilioni 3.398 mwaka 2024/25. Hali hii imechochea pia ongezeko la pato la mwananchi mmoja mmoja kutoka shilingi 1,588,604 hadi 1,710,562 katika kipindi hicho.

“Katika ukusanyaji wa mapato, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Singida imeongeza makusanyo kutoka shilingi bilioni 11.9 mwaka 2021/22 hadi bilioni 30 mwaka 2024/25, ongezeko la asilimia 152. Kwa upande wa mapato ya ndani ya halmashauri, ongezeko limefikia asilimia 69.8, kutoka shilingi bilioni 14.6 mwaka 2020/21 hadi bilioni 24.8 mwaka 2024/25,”ameeleza.

Katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na uhakika wa chakula na kipato, amesema Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya kilimo na ufugaji ambayo inategemewa na zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Singida. Mkoa umefanikiwa kujitosheleza kwa chakula kwa kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 649,850 hadi kufikia tani 1,325,201 kwa mwaka.

Amefafanua kuwa usajili wa wakulima kupitia mfumo wa M-Kilimo umeongezeka kutoka wakulima 75,398 mwaka 2020/21 hadi 293,385 mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 289. Matumizi ya mbolea yamepanda kutoka tani 1,772.5 hadi tani 7,948.75, sawa na ongezeko la asilimia 348.4, huku matumizi ya mbegu bora yakiongezeka kutoka tani 625.5 hadi tani 1,397.2 – sawa na asilimia 123.4.

Katika sekta ya umwagiliaji, jumla ya hekta 17,437 kati ya 48,619 zinazofaa zinatumika kwa umwagiliaji kupitia skimu 24 zilizosajiliwa rasmi na Tume ya Umwagiliaji. Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 81 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji katika mkoa huo.

UTAWALA BORA NA HAKI ZA KIJAMII

Katika kuhakikisha huduma za Serikali zinaimarika, Mkoa umeajiri jumla ya watumishi wapya 2,506 na kuwapandisha vyeo watumishi 5,179 waliokuwa na sifa. Serikali imelipa malimbikizo ya mishahara yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.26 na posho kwa Waheshimiwa Madiwani zaidi ya shilingi bilioni 9.16.

Kwa upande wa utoaji wa haki na msaada wa kisheria, wananchi 513,117 wamefikiwa kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid huku kituo jumuishi cha msaada wa kisheria kikiendelea kujengwa mkoani humo. Ufanisi katika mikutano ya kijamii umeongezeka ambapo vikao vya WDC vimepanda kutoka 76.5% hadi 95%, mikutano ya vijiji kutoka 64% hadi 88% na mikutano ya wakazi wa mitaa kutoka 35% hadi 98% ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Kwa upande mwingine amezungumzia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF),ambapo ameeeleza kaya 57,012 zimeendelea kunufaika kwa kupata ruzuku ya shilingi bilioni 47.942, ambapo kaya 12,130 kati ya hizo zimeondokana na umasikini uliokithiri.

Aidha amesema mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vikundi imefikia shilingi bilioni 5.686 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hatua inayochochea ujasiriamali na ajira za ndani.

Kuhusu takwimu za mkoa naa mchango wa wananchi,ameeleza kuwa Mkoa wa Singida una wakazi 2,008,058, wakiwemo wanaume 995,703 na wanawake 1,012,355. Idadi hii inaonyesha ongezeko la watu 637,421 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, sawa na asilimia 3.8.

“Kiusimamizi, mkoa umegawanyika katika wilaya tano ambazo ni Singida, Manyoni, Iramba, Mkalama na Ikungi, na una jumla ya halmashauri saba: Singida, Manyoni, Itigi, Mkalama, Iramba, Ikungi na Manispaa ya Singida, ” ameeleza.

Aidha Dendego amewataka wananchi kuendeleza mshikamano na ushirikiano na Serikali ili kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanakuwa endelevu, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

“Mafanikio haya si ya Serikali peke yake bali ni ushindi wa wananchi wote wa Singida. Ushirikiano wenu ndiyo msingi wa kasi ya maendeleo tunayojivunia leo,” amesema Dendego.