Soko la mabilioni kuchochea uchumi Tarime

Na Immaculate Makilika- MAELEZO

Mkurugenzi Mtendaji wa Mji Tarime, Gimbana Ntavyo anasema kuwa ujenzi wa soko la kisasa unaoendelea mkoani Mara katika halmashauri yake utasaidia kuchochea biashara katika Mji wa Tarime pamoja na kutoa fursa ya kufanya biashara na nchi jirani ya Kenya na hivyo kukuza uchumi wa wananchi wake.

Akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa makala hii, hivi karibu wilayani Tarime, Mkurugenzi huyo anasema kuwa soko hilo la kisasa ambalo ujenzi wake unaendelea, limefika asilimia 68 na linatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.

Ujenzi wa soko la kisasa unaoendelea katika Halmshauri ya Tarime Mji mkoani Mara ambao umefikia asilimia 68 na unatarajia kukamilika Julai mwaka 2023.

“Soko hili hadi kukamilika kwake litagharimu kiasi cha shilingi 9,680.916, 574.99 na hadi sasa halmashauri imepokea kiasi cha shilingi 4,784,523,065.37 sawa na asilimia 49.4 na imeshalipa kiasi cha shilingi 3,948,831,242.00 sawa na asilimia 40.8.

Aidha, soko hilo linatajwa kutoa jumla ya ajira 441 kwa wananchi na kuwa mradi huo utakapokamilika utakuwa na maduka ya nje 134, maduka ya ndani 188, vizimba 160, maduka ya nyama matatu, migahawa miwili, duka kubwa moja na benki mbili.

Mhandisi Mshauri wa mradi huo wa ujenzi wa soko, Leonard Mwangoka kutoka kampuni ya Mhandisi Consultant analeza kuwa ujenzi wa soko ulianza Januari 19, 2022 na umezingatia ubora wa viwango wa vifaa vinavyotumika ili soko lidumu kwa muda mrefu.

“Mradi huu pia umezingatia watu wenye mahitaji maalum na hivyo utakapokamilika utakuwa na miundombinu ya watumiaji wa viti vya magurudumu ili kuwasaidia kuingia na kutoka sokoni”, anaeleza Mwangoka.

Mkazi wa Tarime, Bi. Agnes Julius anasema “Nimefurahia mradi huu unasaidia, napata kipato kwa kuwa hapa nafanya kazi za usaidizi kama kubeba zege na hivyo napata fedha kwa ajili ya kutunza familia yangu”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Tarime, Gimbana Ntavyo.

Naye, Bw. Mwai Mjinja anayefanyakazi katika mradi wa ujenzi wa soko hilo anasema, “kwa kweli tunashukuru kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutuletea miradi mingi na vijana wengi tunapata fursa za ajira katika miradi mbalimbali anayoitekeleza”.

Mjasiriamali, Bi. Beatrice Okore anasema uwepo wa mradi wa soko hilo unaleta matumaini kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa Tarime kwa kuwa itaboresha mazingira yao ya kufanyia kazi.

“Kwa kweli soko hili likikamilika itakuwa faida sana kwetu, kwa sasa tunafanyakazi katika mazingira magumu na wateja wetu wanazunguka maeneo mbalimbali kutafuta bidhaa, lakini soko likiisha na tukiwa pale itawarahisishia kupata bidhaa mbalimbali kwa urahisi na katika sehemu moja, anasisitiza Beatrice.