Na Mussa Augustine,JamhuriMedia

Soko la Kimataifa la Samaki Feri lililoko Kivukoni jijini Dar es Salaam linakabiliwa na changamoto ya kuwa na idadi kubwa ya wafanyabiashara zaidi ya 3000 huku uwezo wake halisia ni kuwa na uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara wapatao 1500 hadi 2000 pekee.

Akizungumza Dar es Salaam Januari leo Januari 17,2023 katika mahojiano maalumu na JAMHURI DIGITAL wa meneja wa soko hilo Denis Mrema amesema kuwa kuongezeka kwa wafanyabiashara hao kunachangia kuharibika kwa miundombinu ya soko hilo mara kwa mara.

Meneja wa soko la Feri, Denis Mrema akizungumza na mwandishi wa habari (Hayupo pichani)

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt.Samia Suluhu Hassan inatarajiwa kujenga soko moja kila wilaya ili kuondoa adha inayojitokeza kwenye masoko yaliyopo kwa Sasa.

Mrema amesema kuwa uongozi wa soko hilo una mikakati mizuri ya kuhakikisha wafanyabiashara hao wananufaika na mikopo kutoka taasisi za kifedha ikiwemo benki, pamoja na mikopo ya asilimia 10 inayotengwa kila halmashuri kwa ajili ya mikopo kwa vijana,wanawake na wenye ulemavu,hivyo wafanyabiashara hao amewaomba kupitia viongozi wao wa wadau wa soko kuhakikisha wanawasilisha kwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilala, majina ya watu wote wanaotaka mikopo.

Sanjari na hayo amesema kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya wafanyabishara lakini wanaendelea kujitahidi kuhakikisha suala la usafi wa soko unafanyika ipasavyo ili kuzuia Magonjwa ya mlipuko ambapo kuna gari taka linalotoa huduma kila wakati ,nakwamba changamoto iliyopo ni upatikanaji wa mipira,magadi, sabuni,blashi, gloves,mifagio,pamoja na matoroli ili kuifanya kazi ya mzabuni wa taka sokoni hapo kuwa nyepesi nakuhakikisha usafi unafanyika Kwa kiwango kinachotakiwa.

Wafanyabiashara wa dagaa soko la samaki Feri

“Soko hili limekuwa likijiendesha kupitia mapato tunayokusanya,mimi na vijana ninaosaidiana nao kukusanya ushuru tunaangalia na kujiwekea malengo ya kukusanya kwa mwaka na kugawanya kwa miezi 12 kila mwezi tukusanye kiasi gani, hivyo tunahakikisha pia kila mwisho wa mwezi tunapeleka asilimia 30 ya mapato katika halmashauri Kwa ajili ya shughuli za maendeleo,na hatujawahi kuacha kupeleka “amesema Mrema.

Amesema kuwa soko hilo limefanikiwa kuongeza kina cha maji na kuzifanya boti za uvuvi kufanya kazi yake vizuri,pia soko hilo linatarajia kujenga jengo kubwa la kisasa kwa ajili ya kupumzika wavuvi wanapotoka baharini kuvua samaki ambapo tayari tenda ya kutafuta mzabuni imeshatangazwa na Halmashauri ya Manisapaa ya Ilala,nakwamba pia halmashauri hiyo mwishoni mwa mwaka 2022 imepeleka sokoni hapo injini ya boti inayofanya doria na kulinda mazao ya baharini.

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabishara wa soko hilo Tausi Isaya ambaye ni mamalishe na Obed Samueli ambaye ni baba lishe katika soko hilo,kwa nyakati tofauti wamesema kuwa mfumuko wa bei ya vyakula uliopo kwa sasa unasabbisha wasipate faida kwenye biashara wanazofanya, nakwamba pia kuna baadhi ya Wafanyabiashara wa chakula kutoka nje ya soko wanakuja kufanyabiashara ndani ya soko hilo hali inayochangia pia wafanye biashara katika mazingira magumu.

Naye Katibu wa Zone namba 4 ya Mama na Baba lishe Said Maalim Idd,amesema kwamba hali ya mfumuko wa bei umechangiwa na Vita vya Ukraine na Urusi vinavyoendelea kwa sasa hivyo ametoa wito kwa uongozi wa Halmashauri ya Ilala kutatua kero zinazowakabili ikiwemo suala la baadhi ya wafanyabiashara wanaotoka nje ya soko kufanya biashara ndani ya soko ,pia kupatiwa mikopo Kwa wakati pindi wanapohitaji.

Hata hivyo Meneja wa Soko hilo ameahidi kufanyia kazi changamoto hizo huku akiwataka Wafanyabiashara wa soko hilo kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku wakitambua kuwa Serikali ipo nyuma yao na inahakikisha inawatengenezea mazingira mazuri yakufanyia biashara.

By Jamhuri