Tahadhari kwa Mikoa Hii Itakumbwa na Mvua Kubwa

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imewataka wananchi kuchukua tahadhari juu ya uwepo kwa vipindi vya mvua kubwa katika maeneo yote ya pwani kuanzia leo usiku mpaka Aprili 16, mwaka huu.

Mikoa iliyotajwa kuwa na vipindi vya mvua kubwa ni pamoja na Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Katika tarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo leo, imeeleza kuwa maeneo yaliyotajwa yanatarajiwa kuwa na vipindi vya mvua kubwa iinayozidi milimita 50.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa hali hiyo imesababishwa na kuimarika kwa ukanda wa mvua (Inter-Tropical Covegence Zone ITCZ).

Maeneo tajwa, yameshapata vipindi vya mvua kubwa, hivyo ongezeko la mvua linaweza kusababisha madhara.

Wakazi wa maeneo tajwa wameshauriwa kuchukua tahadhari stahiki na kuendelea kufuatilia taarifa pamoja na tahadhari zinazotolewa.