‘Tangu uhuru usafiri wetu ulikuwa wa mitumbwi na boti tu’

Na Muhidin Amri,JamhuriMedia,Nyasa

Wakazi wa kijiji cha Ndonga, Kata ya Liwundi, Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, wameishukuru Serikali kwa kujenga barabara mpya inayounganisha kijiji hicho na Njambe ambayo imesaidia kuondoa kero za muda mrefu zilizosababishwa na kukosekana kwa barabara ya uhakika.

Wamesema hayo jana mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas, aliyefika katika kijiji hicho kwa ajili ya kukagua ujenzi wa barabara inayoanzia kijiji cha Njambe hadi Ndonga yenye urefu wa km7.

Barabara hiyo inajengwa na Wakala wa Barabara za mjini na vijijini(TARURA) kwa gharama ya zaidi ya Sh.milioni 220, ambapo itaharakisha shughuli za uchumi na uzalishaji mali hasa kusafirisha dagaa kutoka ziwa nyasa kwenda maeneo mengine ya Tanzania.

Marietha Mkondola alisema, katika kijiji hicho hakukuwa na huduma yoyote ya mawasiliano ya barabara tangu uhuru mwaka 1961,badala yake wananchi walipotaka kusafiri kwenda maeneo mengine wakiwamo watumishi wa umma walilazimika kutumia mitumbwi na boti hali ambayo imechelewesha sana uchumi wao.

Mkondola amesema,kukamilika kwa barabara hiyo sasa kutasaidia hata makazi yao hasa ardhi kuwa na thamani kubwa na kuongezeka kwa idadi ya watu watakaokuwa wanaitumia kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Amesema,tangu Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani mwaka mmoja uliopita,wameshuhudia maendeleo makubwa katika kijiji chao ambapo serikali imejenga na kuboresha huduma za kijamii ikiwamo umeme na barabara.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo imeiangalia barabara hiyo kwa jicho la pili kwani wananchi walikuwa wanapata changamoto kubwa ya usafiri pindi wanapohitaji kwenda maeneo mengine.

Amesema,serikali inafanya kazi kubwa ya kutatua kero mbalimbali katika sekta ya barabara,umeme na nyingine kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kujenga na kukarabati barabara kwa lengo la kurahisisha huduma ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa ili kukuza uchumi.

Amesema,kijiji hicho kilikuwa kama kisiwa kwa sababu kukosekana kwa mawasiliano ya barabara ambapo alitolea mfano,kwenda makao makuu ya kata Liundi walilazimika kutumia mitumbwi ambayo wakati mwingine haikuwa salama.

Amewataka wananchi wa kijiji cha Ndonga kutambua kuwa barabara hiyo ni yao,hivyo wana wajibu wa kuilinda kwa ari na mali ili iweze kudumu kwa muda mrefu na waitumie kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo.

Kanal Laban,amemuagiza Meneja wa TARURA wilaya ya Nyasa Mhandisi Thomas Kitusi, kuhakikisha inafanya marekebisho kwa baadhi ya maeneo ambayo yatajengwa makalavi.

Meneja wa Tarura wilayani Nyasa Thomas Kitusi amesema,barabara hiyo inaunganisha kata ya Kihagara na Liwundi hadi sasa wametumia kiasi cha Sh.milioni 220,305,000.00 kuifungua barabara hiyo katika kipindi cha miaka miwili ambapo awali katika kijiji hicho hakukuwa na mawasiliano yoyote ya barabara.

Amesema,tangu uhuru barabara hiyo haikupitika na hivyo wananchi wa kijiji hicho hawakuwahi kuona gari,na usafiri pekee ulikuwa mitumbwi na boti na kuishukuru serikali kwa kutoa fedha ambazo zimetumika kufungua barabara hiyo.