Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

WAKALA wa Barabara mkoani Pwani (TANROADS), imeanza kuchukua tahadhari ya ujio wa mvua ya el nino ikiwa ni hatua za awali kufungua kingo katika madaraja 318 na makaravati 1,540.

Akitembelea kuona kazi zinazofanywa kwenye baadhi ya madaraja ya Mdaula, Msufini katika barabara kuu ya Morogoro na Chalinze-Segera ,Meneja wa TANROADS Pwani ,Mhandisi Baraka Mwambage alieleza ,kati ya madaraja hayo 318 madaraja 20 kazi imekamilika.

Alieleza, huo ni utekelezaji baada ya kupata maelekezo ya Serikali wameanza kuchukua tahadhari kama mkoa.

Mwambage alieleza, wameamua kutoa kipaombele kufukua kwa kufungua maeneo ya kuingia na kutokea kwenye madaraja hayo ili kuruhusu maji yapite kirahisi , kujiepusha na mafuriko.

“Sisi Tanroads Pwani tumeanza kufanya ukarabati madaraja 318 na makaravati 1,540 ,ikiwa ni hatua za awali, ya matengenezo kinga ya kufukua kufungua maeneo ya kuingia na kutokea”

Aidha , Mwambage alieleza katika mwaka wa fedha wa 2023/24 , Jumla ya sh. Bilioni 18.980 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya Barabara Kuu na madaraja Mkoani humo.

“Katika mgawanyo huo kiasi cha milioni 950 ni kwa ajili ya matengenezo ya madaraja 318 na makalvati 1,540 “:;Matengenezo kinga ya madaraja yaliyokamilika ni sehemu tu ya utekelezaji wa matengenezo ya madaraja utakaokamilishwa mwezi June 2024 katika mwaka wa fedha wa 2023/24.”

Mwambage alibainisha ,sio kweli kuwa matengenezo kinga yamegharimu sh.milioni 950, matengenezo yote yaliyopangwa katika madaraja hayo kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 yatagharimu milioni 950.

Akiwa eneo la daraja la mto Ngerengere Mwambage alieleza, katika eneo hilo kazi imekamilika baada ya kufukua kipande cha mita 100 na mita nyingine 60 upande mwingine.

Katika daraja la Mazizi , Meneja huyo alifafanua ni moja ya eneo ambalo lilikuwa korofi kipindi cha nyuma ambapo ilisababisha kufunga na kukatika kwa barabara .

Vilevile alitembelea daraja la Lukugira lililopo mpakani mwa mkoa wa Pwani na Morogoro kupitia Bagamoyo na Mvomero , Mwambage alisema ni sehemu ambayo pia inaimarishwa kwa kuwekwa zege lenye nondo ili kuzuia maji.

Kadhalika ,katika kipindi chote cha mvua watakuwa wakiangalia kama kuna madhara na kuchukua hatua kulingana na matatizo yatakayojitokeza.

Mwambage alitoa tahadhari kwa wananchi kwamba, kipindi cha mvua wawe makini pale watakapoona mafuriko, maji yamejaa barabarani wasipite ,na watoe taarifa ili hatua zichukuliwe .

Hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa tahadhari kushuhudiwa kwa mvua kubwa ya El nino ambayo inatarajia kuanza Octoba- Disemba mwaka huu 2023 ambapo itasababisha madhara makubwa ya binadamu na mazingira,mafuriko na maporomoko ya ardhi.