Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani

Wakala wa Barabara mkoani Pwani (TANROADS),imetoa mapendekezo ya kiasi cha fedha sh.bilioni 52.378 katika mwaka wa fedha 2023/2024 ikiwa ni mpango kazi wa matengenezo ya barabara na miradi ya maendeleo.

Aidha, TANROADS Pwani,imefanya kazi kubwa kutekeleza mradi wa kupendezesha miji kwa kuweka taa za barabarani ambapo baadhi ya wilaya taa zimeshawashwa na wilaya nyingine wapo hatua za mwisho za umaliziaji.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya matengenezo kuanzia Julai 2022 hadi Februari mwaka 2023 ,kazi ya miradi ya maendeleo Julai 2022 hadi Februari 2023 pamoja na mapendekezo ya mpango wa bajeti ya miradi ya matengenezo ya miradi ya maendeleo 2023 hadi 2024 ,katika kikao Cha maendeleo ya barabara Mkoani Pwani, Meneja wa TANROADS Pwani , Mhandisi Baraka Mwambage alieleza makisio hayo ni muendelezo wa kufungua mtandao wa barabara Mkoani humo.

Ameeleza ,kwa matengenezo wanalenga kutumia kiasi cha sh.bilioni 26.589 na maendeleo kwa miradi ya mkoani Bilioni 25.789 fedha ambayo haihusiani na miradi mikubwa .

Vilevile Mwambage amefafanua miradi yote ambayo ipo katika vipaombele vya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na maelekezo mahsusi ya viongozi wa Serikali itatekelezwa mwaka wa fedha 2023/2024.

“Mradi kama ule wa daraja la kisasa la Wami limekamilika, Chalinze -Utete hii ni barabara iliyotolewa maelekezo na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, mradi mwingine ni Kwala ambao umekamilika”alibainisha Mwambage.

Hata hivyo ameeleza kuwa,ipo miradi iliyopo kwenye hatua ya usanifu,ikiwemo Bungo-Nyamisati inayoelekea Mafia, Kisiju km.19,Kibaha Hadi Kisarawe na Mkongo kuelekea Ikwiriri.

Nae Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge, ameeleza katika kufungua wilaya ya Rufiji, mchakato wa matengenezo ya barabara ya Chalinze -Utete,hali ilivyo sasa itaanzia Chalinze -Magindu, Nyerere hydro power project kupita daraja kubwa hadi Utete.

“Kwa sasa katika kufungua Wilaya ya Rufiji tutakuwa na barabara tatu Chalinze -Utete, Kisarawe -Maneromango hadi Mloka na Kibiti- Rufiji.”amesema Kunenge.

Pamoja na hayo,Kunenge amezitaka Halmashauri ziongeze kasi katika kupanga miji ,ili kuupa nguvu mkoa kuweza kuomba fedha Serikalini za kutengeneza barabara zaidi za lami.

“Miji inajengwa pembeni ya barabara,kama tutafanya mipango miji vizuri, kupanga miji yetu,tupate barabara,tuingie ndani haiwezekani kuwa na miji isiyokuwa na barabara, “;Tufanye mpango wa makusudi kupanga miji,tuingie ndani, barabara Kuu ibaki kwa ajili ya magari makubwa, tupunguze msongamano, haiwezekani tuwe na miji ambayo haina barabara,na haiwezekani kutumia fedha za Serikali bila kupanga miji yetu”alisisitiza Kunenge.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo Mohammed Usinga ametaka kujua mpango wa mradi wa kupendezesha miji kwa kuweka taa Bagamoyo, upo hatua gani na utakamilika lini wilaya ya Bagamoyo.

Akitolea ufafanuzi suala hilo, Meneja wa TANROADS Pwani Mwambage, ameeleza kwamba, wanaendelea na mradi huo ambapo wilaya ya Mafia, Kisarawe,Kibaha tayari wameshawasha taa hizo na kuhusu wilaya ya Bagamoyo, Kibiti na Mkuranga wanatarajia kuwasha taa mwishoni mwa mwezi wa Aprili.

By Jamhuri