Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee amewashitaki wabunge wa majimbo kwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa kwa kutohudhuria vikao vya Bodi ya Barabara ikiwemo kikao cha ushauri cha mkoa RCC bila kutoa taarifa yeyote.

Akizungumza wakati wa kikao hicho amesema kuwa kitendo cha baadhi ya wabunge kutohudhuria vikao hivyo bila sababu za msingi si cha kiuungwana kwani wanapaswa kufahamu kuwa wamechaguliwa na wananchi ili kuwawakilisha maeneo ambayo kimsingi wao ni wawakilishi kama vikao hivi.

“Mimi niseme mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Patrick Chandi, jambo hili wabunge kutohudhuria vikao bila sababu za msingi, wakati wabunge ni wajumbe wa mkutano kama huu niseme hawawatendei wananchi wao haki.

“Nikuombe mwenyekiti kama wabunge hawatakuwa wanahudhuria vikao kama hivi Serikali iwafutie posho wanazochukua za vikao kama hivi na jambo hili nimelipigia kelele sana lakini hakuna kinachofanyika isionekane kuwa nina maslahi na leo ndio mwisho katika kulizungumzia jambo hili ”amesema Mzee.

Katika kikao hicho mkuu wa mkoa Mara ameonekana kukerwa na baadhi ya taarifa ambazo zinaandaliwa kwa wajumbe bila kuwa na changamoto ambazo zinalalamikiwa na wananchi katika maeneo mbalimbali ili kupatiwa ufumbuzi badala yake wahusika wanaandaa taarifa za mafanikio peke yake jambo ambalo kimsingi zinakuwa za upande moja.

Mzee alitumia nafasi hiyo kuwashawishi wajumbe kuridhia wazo la kutafuta eneo la kujenga stendi ya kisasa ya magari stendi ambayo kwa Mkoa wa Mara haipo na kuwa kujengwa kwa stendi hiyo kutainua uchumi kwa wafanyabiashara na pia hadhi ya mkoa itapanda lengo la kuinua mapato.

Mmoja wa wadau wa maendeleo ambaye pia ni mjumbe wa kikao hicho,Mordekai Moseti ameomba kuunda vikundi na kubainisha vilivyopo vya asilimia 30 kwa lengo la kuongeza vikundi kuwa vingi na kupaisha makusanyo ya mapato ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwenye mkoa badala ya kutegemea keki ya Serikali hali ni kidogo.

Kwa upande wake Meneja Wakala wa Barabara Mkoa Mara(TANRORD),Vedastus Maribo amewambia wajumbe kuwa jumla ya shilingi 17,402,185,000.00 zimeombwa kutoka mfuko wa barabara kwa ajili ya kugharimia matengenezo ya barabara katika makisio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2023-2024.

Mbunge wa jimbo la Tarime mjini,Michael Kembaki ameonyesha kukerwa na baadhi ya wananchi wanaoharibu miundombinu ya barabara kama vile kupitisha mifugo,uvamizi wa hifadhi ya barabara na wizi wa miundombinu kwa makusudi huku akiomba sheria kuchuka mkondo wake dhidi ya watu kama hao.

Naye meneja TARURA Mkoa wa Mara,amesema wana mtandao wa barabara wenye urefu wa jumla kilomita 4539.98 kati ya hizi barabara za muunganisho(Collecor) ni kilomita 1965.77 barabara za mlisho (Peeder) ni kilomita 2205.18 na barabara za vijiji(Community)ni kilomita 388.18 vilevile TARURA Mara ina idadi ya madaraja 139 na makalavati 2617