Tanzania na Zambia zimekubaliana kutatua changamoto za usafirishaji wa mizigo baina ya nchi hizo hususani foleni ya maroli katika eneo la Tunduma ili kupunguza gharama na muda kwa wasafirishaji.

Akizungumza mara baada ya kikao cha cha Makatibu Wakuu, Wataalam na Wasafirishaji mkoani Songwe, Katibu Mkuu Uchukuzi, Gabriel Migire amesema suluhu ya kupunguza foleni katika mpaka huo kutarahisisha shughuli za usafirishaji wa mizigo na hivyo kuruhusu mzigo kumfikia mlaji kwa wakati. 

“Changamoto katika usafirishaji ziko nyingi lakini kwa mpaka huu changamoto kubwa ni foleni ambapo madereva hukaa muda mrefu, hali hii inaongeza sana gharama za usafirishaji hivyo kikao cheti cha siku mbili hapa lazima tutoke hapa na majawabu’ Amesema Katibu Mkuu Migire.

Katibu Mkuu Migire ameongeza kuwa kikao hicho cha nchi mbili kimehusisha wataalam na wasafirishaji ili kujadili kwa kina changamoto zote ili kufanya wasafirishaji wengi zaidi kutumia mpaka huo wa Tunduma bila usumbufu.

Aidha, Katibu Mkuu Migire ameogeza kuwa moja ya makubaliano yaliyoafikiwa katika kikao hicho ni pamoja  kuboresha sehemu za maegesho ya magari kwa pande zote mbili ili kurahisisha uingiaji na utokaji wa magari mpakani.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Sekta ya Uchukuzi na Logistic kutoka Zambia Mwalusaka Fredrick amesema kwa upande wa Zambia kuna changamoto ya miundombinu wezeshi ikiwemo barabara, skana za kukagua mizigo na uhaba wa watumishi mpakani na kuahidi kuzitatua kwa haraka ili kutokwamisha jitihada zinazoendelea za kurahisisha usafirishaji mpakani  hapo.

Naye Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Mrisho Mrisho  amesema suluhu ya changamoto za mpaka wa Tunduma zitaongeza ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam kwani mzigo utapakuliwa na kuondoka bandari hapo na kuwafikia walaji kwa wakati.

By Jamhuri