WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ,kupitia shamba la miti la Sao Hill lilopo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wamefanikisha mashindano ya magari ya mbio fupi ya Sao Hill Auto Cross ambayo yalikuwa kivutio kikubwa kwa wananchi wa mkoa wa Iringa na nje ya mkoa wa Iringa waliofika katika eneo ambalo mashindano yalifanyikia

Akizungumza baada ya kuzinduliwa rasmi kwa mashindano hayo katika Shamba la Miti Sao Hill linalomikiliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS), Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo Lucas Sabida amesema ndio mara ya kwanza kwa Wakala huo kuandaa mashindano hayo ikiwa ni utalii mpya ambao wameutambulisha kwenye sekta ya utalii nchini.

“Katika shamba la Sao Hill fursa ziko nyingi , tunazalisha bidhaa zinatokana na mbao , asali na tunazo fursa za uwekezaji.Sasa tumekuja na utalii wa michezo kwenye maeneo yetu ya hifadhi za misitu ya asili na ile misitu ya kupanda kama Sao Hill kama ambavyo leo tumeanza na mbio fupi za magari.

Mmoja ya magari ambayo yaliyoshiriki Mashindano ya mbio fupi za magari zilizofanyika katika Shamba la Miti Sao Hill

“Sao Hili tunalo eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 155,000 na zina barabara zenye urefu wa kilometa 1,500 kwa hiyo ukiunganisha hizi barabara unaweza kutoka hapa(Sao Hill) hadi Mwanza .Hivyo tunaweza kufanya mashindano makubwa ya ya magari hata ya Bara la Afrika,”alisema.

Ameongeza katika shamba la Miti Sao Hill inawezekana kufanyika michezo ya aina yoyote kwani kuna eneo kubwa na la kutosha lakini TFS wameamua kuanza na mashindano ya magari ambayo wanatarajia yatakuwa yakifanyika kila mwaka kwa kushirikiana na wadau wengine.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Saad Mtambule mkoani Iringa alisema utalii wa mashindano ya mbio za magari kwenye Shamba la Sao Hill unakwenda kufungua fursa zaidi katika sekta ya utalii na wao wamejiandaa kupokea wananchi na wawekezaji walio tayari kufanya uwekezaji kwenye sekta ya utalii.

Alisema sekta hiyo imeendelea kukua kwa kasi kubwa kutokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipotangaza utalii kupitia filamu ya Royal Tour.


Mshindi wa Pili katika Mashindano ya mbio fupi za magari zilizofanyika katika Shamba la Miti Sao Hill Ahamed Mbatta ( wa kwanza kushoto) akikabidhiwa Kikombe cha ushindi na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Saad Mtambule ( wa pili kulia).Aliyeshika kipaza sauti ni Mchezaji wa mbio hizo John Makeo.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa kuanzisha filamu ya Tanzania Royal Tour na sisi kupitia sekta ya misitu tumeona pamoja na kupata mbao na kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na misitu tunaamini mashindano ya magari yataongeza fursa na kuleta bidhaa mpya kwenye sekta ya misitu .

“Pia tunawapongeza TFS kupitia Shamba la Miti Sao Hill pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii ikiongoza na Balozi Pindi Chana kwa uratibu mzuri wa mashindano haya ya magari yanayofanyika hapa. Kwetu mashindano haya ya magari yanakwenda kuongeza fursa nyingine kwa wananchi wetu,”amesema.

Kwa upande wa Mchezeshaji wa Mbio hizo za magari John Makeo alisema mashindano hayo yamefanyika ya kilometa sita na kila mzunguko ulikuwa ni kilometa 1.5.“Mbio fupi lengo lake ni kuwaanda madereva wa kesho na keshokutwa , kikatiba mbio hizo zinatakiwa kuchezwa kilometa moja, isizidi kilometa 1.5.”

Mshindi wa kwanza katika Mashindano ya mbio fupi za magari zilizofanyika katika Shamba la Miti Sao Hill Faraj Abri( wa pili kushoto) akikabidhiwa Kikombe cha ushindi na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Saad Mtambule ( wa pili kulia).Aliyeshika kipaza sauti ni Mchezaji wa mbio hizo John Makeo.

Aidha alisema Sao Hill kuna maeneo mazuri kwa ajili ya kufanya mashindano ya mbio za magari hasa kwa kuzingatia kuna eneo la kutosha na bahati nzuri hakuna makazi ya watu zaidi ya msitu ulitokana na miti ya kupandwa na miti asili

By Jamhuri