Kwa muda sasa MM amekuwa haonekani. Kuna maswali mengi juu ya kupotea kwake, lakini anawahakikishia wasomaji kuwa bado yupo, ukiachilia mbali matatizo ya kiafya ya hapa na pale yanayosababishwa na umri wake.

Ni kwa sababu hizo hizo za umri, MM amekutana na kituko ambacho hana hakika kama kimebarikiwa na uongozi wa Manispaa ya Kinondoni, au uongozi huo hauna taarifa.

Wiki iliyopita MM alikwenda kutibiwa katika Zahanati ya Msewe iliyo jirani na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Nyuma ya hiyo zahanati, MM akashangazwa na kundi kubwa la vijana na watu wazima waliobanana kweli kweli kwenye ukuta eneo la uani.

MM alipouliza, akaambiwa kundi hilo lipo usiku na mchana kwa sababu watu wanakwenda hapo kujiunga na mitandao ya simu ili kupata vile vifurushi vya tIGO ambavyo mtumiaji wa simu huweka Sh 1,500 na akishajiunga anapiga simu kwa wiki nzima. Ofa hiyo ni mahsusi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu. Wanachofanya wananchi hao ni kwenda hapo ili waweze kujiunga, na eneo pekee ambalo mtandao unapatikana ni nyuma katika madirisha ya wodi na chumba cha uzazi. MM akaambiwa Zahanati ya Msewe kwa sasa ina vifaa vyote vinavyohusika kwa utoaji huduma kwa wajawazito wanaojifungua, lakini huduma hiyo imekwama kwa sababu watu ‘wamehamia’ hapo nyuma ya chumba za uzazi, na kuibua kero kubwa.

MM akaambiwa mpango unaofanywa sasa ni wa kujenga uzio (ukuta) ili kusaidia kuzuia watu wanaofika hapo kujiunga kwenye vifurushi wasione kinachoendelea katika chumba cha uzazi na wodi ya wajawazito.

Hadi hapo MM akawa amepigwa na butwaa kuona kinamama wanapata tabu kwa kukosa huduma ya kujifungua kwa sababu chumba cha uzazi kimevamiwa na genge la wanafunzi na watu wanaopenda vya bure. MM ameona hili si jambo la kawaida. Akaonelea vyema aiambie Manispaa ya Kinondoni kuwa ukuta unahitajika haraka mno Zahanati ya Msewe ili kuifanya wodi na chumba cha wazazi vianze kufanya kazi. Haya ndiyo madhara ya vifurushi vya bure vya tIGO eneo hili la Msewe!

By Jamhuri