TMA yatoa ushauri wa kupanda mazao yanayokomaa muda mfupi

Na Stella Aron,JamhuriMedia,Dar

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imewashauri wakulima kupanda mazao na mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi na zinazostahimili upungufu wa mvua kama vile mazao jamii ya mizizi, mikunde na mazao ya bustani.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma ya Hali ya Hewa Dkt. Hamza Kabelwa akitoa mwelekeo wa Mvua za Msimu (Novemba, 2022 hadi Aprili, 2023) jijini Dar es Salaam.

Ushauri huo umetolewa na jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma ya Hali ya Hewa Dkt. Hamza Kabelwa wakati akitoa mwelekeo wa Mvua za Msimu (Novemba, 2022 hadi Aprili, 2023).

Kabelwa amesema ushauri huo unatokana na Utabiri wa Mvua za Msimu kuonyesha kuwepo kwa mvua za chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi yanayopata mvua za msimu ambazo zinaweza kusababisha upungufu mkubwa wa unyevunyevu katika udongo katika msimu huu.

Pia ameshauri kutumia mbinu na teknolojia bora za kilimo himilivu za kuhifadhi maji na unyevunyevu wa udongo ikiwa ni pamoja na uvunaji wa maji ya mvua na matumizi ya matandazo.

“Kulima mazao yanayohimili ukame na kuhifadhi maji na unyevunyevu wa udogo ni njia mojawapo ya kusaidia wakulima kuvuna mazao kwa wingi na kuwepo kwa akiba ya chakula,” amesema.

Katika kufanikisha utabiri huo ni vyema sasa wakulima na maafisa ugani wakazingatia ushauri na tabiri zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo.

Akizungumzia kuhusu mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, amesema mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Kwamba mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa na Kusini mwa mkoa wa Morogoro.

Kwamba katika nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2022-Januari 2023) vipindi virefu vya ukavu vunatarajiwa kujitokeza.
Ameeleza kwamba ongezeko la mvua linatarajiwa katika nusu ya pili ya msimu (Februari-Aprili, 2023).Aidha amesema mvua za nje ya msimu zinatarajiwa mwezi Mei, 2023 katika maeneo mengi.

Amebainisha kwamba maeneo ya mikoa ya Singida na Dodoma mvua za Msimu zinatarajiwa kuanza kwa kuchelewa katika wiki ya pili ya mwezi Januari, 2023.