Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Stanslaus Nyongo ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuongeza nguvu ya kudhibiti bidhaa feki za dawa zinazoingia nchini Tanzania.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Nyongo ameyasema hayo leo Agosti 17, 2023 baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TMDA Bw. Adam Fimbo katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kilichofanyika Bungeni Jijini Dodoma.

“Tunaona juhudi mnazofanya za kuteketeza dawa feki zinazoingia nchini, hii inaonesha bado kuna mianya mingi ya kuingiza dawa nchini hivyo ni muhimu sana kuongeza nguvu ya kudhibiti uingizwaji wa dawa feki”, amesisitiza Mhe. Nyongo

Aidha, Mhe. Nyongo ameitaka Mamlaka hiyo kuangalia ufanisi wa dawa zilizopo kwa maana kuna baadhi ya dawa hazina ubora mzuri unaotakiwa kulingana na dawa husika hasa kwenye dawa wa ‘Antibiotic’.

“Kuangalia ufanisi wa dawa iwe kipaumbele cha kwanza hasa kwenye hizi dawa za ‘Antibiotic’, maaana anaweza kuja mgonjwa anasema nikitumia dawa hii inaniponyesha kwa haraka kuliko nikitumia dawa hii, Sasa hii ni changamoto kwenu mkalifanyie kazi”, amesema Mhe. Nyongo

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu katika suala la ubora wa dawa amesema linaangaliwa katika mambo Matatu, Kwanza Ubora, Pili usalama na Tatu ufanisi.

“Kwanza tunaangalia swala la ubora, Pili tunaangalia usalama na Tatu tunaangalia ufanisi, kwa hiyo hapa TMDA mnatakiwa kuongeza nguvu kwenye ufanisi wa dawa”, amesema Waziri Ummy

Pia, Waziri Ummy ameipongeza TMDA kwa jitihada wanazofanya kwenye TEHAMA kwa kuwa hakuna malalamiko yeyote ya mtu kukwama usajili kwa muda wa miaka Miwili”, amesema Waziri Ummy

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Bw. Adam Fimbo amesema, Usajili wa waganga wa tiba asili nchini ulianza Mwaka 2010 ambapo hadi Julai Mwaka 2023, idadi ya wataalam wa Tiba Asili/Mbadala waliosajiliwa ilifikia 47,467 na vituo vya kutolea huduma 1,640 vilikuwa vimesajiliwa.

“Baada ya kufanya usajili huo, matarajio ya Wizara katika kipindi cha mwaka 2023/2024 huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini zitaimarika na kuboreshwa zaidi kwa kuzingatia Sheria na mikakati iliyowekwa na Baraza”, amesema Fimbo.